BENKI ya NMB imefanikiwa kumaliza changamoto ya madawati katika shule ya msingi Mipeta iliyopo katika Kata ya Muhukuru,Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.
Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Songea Frank Rutakwa akizungumza katika kijiji hicho kabla ya kukabidhi msaada wa madawati 150 yenye thamani ya shilingi milioni 10,amesema Benki hiyo imeamua kutoa msaada huo baada ya kupata taarifa kupitia vyombo vya habari kuhusu upungufu wa madawati katika shule hiyo.
Anasema NMB imeamua kushirikiana na shule ya Msingi Mipeta kwa kuchangia madawati imara yenye vyuma na kwamba Benki hiyo imekuwa inapokea maombi mengi ya kuchangia miradi mbalimbali.
Rutakwa amesema changamoto katika sekta ya elimu ni miongoni mwa vipaumbele vya Benki ya NMB kwa kutambua kuwa elimu ni uti wa mgongo wa Taifa lolote hapa duniani.
“Tunatambua juhudi za serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli ya kusimamia elimu kwa nguvu zote na kusaidia kutoa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari’’,anasisitiza Rutakwa.
Anasema mchango wa madawati katika shule hiyo ni kuonesha kwa vitendo ushiriki wa NMB kwa vitendo ili kuhakikisha jamii inayozunguka inafaidika na uwepo wa Benki ya NMB ambayo ipo karibu na jamii.
Amesema kwa miaka kadhaa sasa NMB imekuwa inashiriki katika miradi ya maendeleo kwa kujikita katika sekta ya elimu na afya na kusaidia majanga yanapotokea katika maeneo mbalimbali nchini.
Kulingana na Kaimu Meneja huyo wa Kanda,katika kipindi cha mwaka 2018,NMB imetenga shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya jamii ikiwemo kuchangia sekta ya afya na elimu na kwamba kiasi hicho kinaifanya NMB kuwa Benki ya kwanza kuchangia maendeleo kuliko Benki yeyote nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Mipeta,Henry Kihwili,amesema shule hiyo kata ya Muhukuru ilianzishwa mwaka 2002 ipo umbali wa kilometa 108 toka mjini Songea na umbali wa kilometa 62 toka makao makuu ya kata.
Kihwili anabainisha zaidi kuwa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 354 wanaosoma kuanzia darasa la Awali hadi la sita na kwamba shule hiyo ina jumla ya walimu sita.
Mkuu huyo wa shule ameipongeza NMB kwa msaada wa madawati 150 ambayo yamemaliza changamoto ya upungufu wa madawati katika shule hiyo.
Kihwili anasema kabla ya msaada wa madawati hayo,shule hiyo ilikuwa na upungufu wa madawati 118 ambapo madawati yaliokuwepo yalikuwa ni 103 na kwamba hivi sasa kutokana na msaada wa madawati hayo,hakuna tena upungufu wa madawati katika shule hiyo.
Diwani wa Kata ya Muhukuru Manufred Mzuya anasema kabla ya msaada wa madawati 150 kutoka Benki ya NMB,shule hiyo ilikuwa inakabiliwa na upungufu wa madawati hali ambayo ilikuwa inaathiri taaluma kwa wanafunzi katika shule hiyo.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa