BENKI ya NMB imetoa msaada wa mabati 175 ya geji 28 yenye thamani ya shilingi milioni tano katika shule ya Msingi Ndelenyuma iliyopo katika Halmashauri ya Madaba wilayani Songea mkoani Ruvuma.
Akizungumza kabla ya kukabidhi bati hizo katika hafla ambayo imefanyika katika shule ya Msingi Ndelenyuma, Meneja wa NMB Kanda ya Kusini Janeth Shango amesema kwa miaka kadhaa sasa NMB imekuwa mstari wa mbele kuchangia miradi ya mbalimbali ya maendeleo.
“Mpaka ninavyoongea leo, kwa mwaka huu 2019 pekee,tayari tumetoa misaada yenye thamani ya shilingi milioni 710,tumejikita zaidi kwenye miradi ya elimu na afya’’,amesema Shango.
Hata hivyo amesema katika miradi ya elimu NMB imejikita katika madawati na vifaa vya kuezekea na katika sekta ya afya wamejikita kwenye vitanda na magodoro yake .
Kulingana na Meneja huyo wa NMB Kanda ya Kusini,kwa mwaka 2019 Benki hiyo imetenga bajeti ya zaidi ya shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya jamii katika sekta ya elimu na afya.
Kwa upande wake Mgeni rasmi katika Hafla hiyo Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema ametoa rai kwa watanzania kuitumia Benki ya NMB kwa kuwa imezifikia wilaya zote nchini kwa asilimia 100 na kwamba inatoa huduma za kibenki kwa mitandao ambazo zinapatikana kwa wananchi wengi zaidi mijini na vijijini.
“Mimi kama Mkuu wa Wilaya kwa niaba ya wananchi wa Madaba na Wilaya ya Songea nawashukuru NMB kwa msaada wenu ambao mmekuwa mnautoa kwetu mara kwa mara’’,amesema Mgema.
Hata hivyo amesema NMB imekuwa msaada mkubwa katika wilaya ya Songea ambapo mwaka 2018 walitoa msaada wa vitanda na magodoro katika kituo cha Afya Madaba na kwamba NMB pia ilitoa msaada wa meza,viti na madawati kwa shule za msingi na sekondari zilizopo katika Wilaya ya Songea.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Madaba Vastus Mfikwa amesema msaada huo umekuja wakati muafaka kwa sababu kijiji hicho ni kipya na usajiri wake hauzidi miezi miwili hivyo msaada huo unatatua changamoto ya vyumba vitatu vya madarasa katika shule ya Msingi Ndelenyuma.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Ndelenyuma Beneth Mwamjembe ameishukuru Benki ya NMB kwa msaada huo ambao amesema unakwenda kutatua changamoto ya mradi wa vyumba vitatu vya madarasa unaoendelea katika shule hiyo.
Amesema mradi vya vyumba hivyo ambao ulianzishwa mwaka 2018 bado haujakamilika na kwamba shule hiyo yenye wanafunzi 68, ilianzishwa mwaka 2014.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Serikalini
Oktoba 28,2019
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa