BENKI ya NMB imetoa msaada wa madawati bora 60 na viti vyake 60 kwa ajili ya shule ya sekondari ya Magingo iliyopo katika Halmashauri ya Madaba wilayani Songea mkoani Ruvuma.
Akitoa taarifa ya Benki hiyo kwenye hafla ya kukabidhi vifaa hivyo iliyofanyika katika shule ya msingi Magingo Madaba,Meneja wa NMB Kanda ya Kusini Haji Msingwa amesema NMB pia imechangia viti vya maabara 132 kwa ajili ya shule ya sekondari ya Lipupuma .
Msingwa amesema vifaa vyote hivyo vimegharimu shilingi milioni 8.5 na kwamba katika mwaka 2020,NMB imetenga bajeti ya zaidi ya bilioni moja kwa ajili ya kuchangia maendeleo ikiwemo kusaidia sekta ya afya na elimu.
“NMB itaendelea kuunga mkono juhudi za wadau wake katika kuhakikisha kuwa changamoto za jamii zinapatiwa ufumbuzi katika kujenga afya na elimu bora’’,alisisitiza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Madaba na Diwani wa Kata ya Mkongotemba Vastus Mfikwa akizingumza baada ya kupokea msaada huo ameishukuru NMB kwa kupunguza changamoto ya madawati katika shule mbili za sekondari zilizopo katika kata yake ambapo vifaa hivyo vitasaidia kuboresha elimu katika Kata hiyo.
Amesema shule ya sekondari ya Magingo ni miongoni mwa shule zilizofanya vizuri kwenye mtihani wa Taifa wa kidato cha nne ambapo Halmashauri ya Madaba imekuwa ya kwanza kati ya Halmashauri nane za Mkoa wa Ruvuma na imeshika nafasi ya 23 kitaifa kati ya Halmashauri 185 Tanzania na msaada huo utachochea zaidi katika elimu.
Afisa Elimu Kata ya Mkongotema Edwin Thadei amesema Kata hiyo ina shule mbili za sekondari za magingo na Lipupuma ambazo zilikuwa zinakabiliwa na changamoto ya meza na viti na kwamba msaada wa NMB umepunguza tatizo kwa asilimia 90 baada ya kutoa msaada wa meza,viti na stuli.
“Kabla ya msaada kutoka Benki ya NMB,sekondari ya Magingo na Lipupuma zilikuwa na upungufu wa meza 77,viti 87 na stuli 82’’,alisema.
Akizungumza kabla ya makabidhiano ya vifaa hivyo ,mgeni rasmi kwenye hafla hiyo ,Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema amesema Benki ya NMB imekuwa msaada mkubwa katika Wilaya ya Songea kwa kutatua changamoto katika sekta ya afya na elimu.
Mgema amesema msaada uliotolewa na NMB unakwenda kuchochea ufaulu kwa wanafunzi kwa sababu wanasoma katika madarasa yenye mazingira rafiki ya kusomea ambapo amesisiza kuwa urithi pekee kwa watoto ni elimu.
Antony Mayemba ni mmoja wa wanafunzi katika sekondari ya Magingo ameipongeza NMB kwa msaada huo ambao amesema umepunguza changamoto ya viti na meza kwa wanafunzi.
NMB ina matawi zaidi ya 224 na wateja zaidi ya milioni tatu katika nchi nzima, ikiwa imezifikia wilaya zote kwa asilimia 100,huku ikiendelea kuboresha huduma za kibenki kwa njia ya mtandao ili kufikisha huduma za kibenki kwa wananchi wengi zaidi.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa