UKUSANYAJI wa mapato kwa njia ya mashine za kieletroniki (POS ) katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoa wa Ruvuma umesababisha mapato ya Halmashauri hiyo kuongezeka kwa asilimia 262 hadi kufikia Machi mwaka huu. Mwekahazina Mkuu wa Manispaa hiyo Denis Mwaitete Akizungumza na jopo la wanahabari ofisini kwake mjini Songea amesema kabla kutumia POS makusanyo kwa mwaka yalikuwa ni shilingi bilioni 1.3 kwa mwaka na kwamba baada ya kuanza kutumia POS makusanyo yamepanda kwa mwaka hadi kufikia shilingi bilioni 2.262 kwa mwaka sawa na asilimia 262.
Amesema hadi sasa Manispaa ya Songea imenunua POS 100 ambazo zimesambazwa katika vituo vyote vya kukusanya mapato na kwamba hakuna kituo ambacho kinatumia mfumo wa vitabu na kwamba POS zimerahisisha watumishi na ofisi ya Mkurugenzi kupata takwimu sahihi za ukusanyaji mapato kwa sikuwa, wiki hadi mwezi hali ambayo inasababisha serikali kupata mapato halali na kupunguza upotevu wa mapato ambao ulikuwapo kabla ya kuanza matumizi ya POS.
Mwaitete ametoa rai kwa wananchi wa Manispaa hiyo na watanzania kwa ujumla kuhakikisha wanatumia risiti za kieletroniki ili serikali iweze kuongeza mapato ambayo yanaiwezesha serikali kuwahudumia wananchi wake na kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo kama ilivyo katika Manispaa hiyo ambako kuna miradi mikubwa ukiwemo ujenzi wa Stendi mpya ya mabasi katika eneo la Kata ya Tanga ambayo itaongeza mapato na kuongeza ajira kwa vijana na wanawake.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari wa manispaa ya Songea
Mei 31,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa