Rais Magufuli atoa dawa kutokomeza mbu Songea
SERIKALI imeongeza chachu katika mapambano dhidi ya malaria baada ya kununua lita laki moja za dawa za kuua mbu na kusambazwa kote nchini ili kukabiliana na malaria.
Viuadudu vya kutokomeza mbu wa malaria vinatengenezwa katika kiwanda cha kuzalisha Viuadudu kilichopo Mjini Kibaha mkoani Pwani.
Halmashauri 14 nchini ikiwemo ya Manispaa ya Songea zina viwango vikubwa vya maambukizi ya ugonjwa wa malaria,tayari Manispaa ya Songea imepokea dawa hiyo na hivi sasa yanafanyika maandalizi ya kuanza kupulizia makazi ya wananchi ili kutokomeza ugonjwa huo.
Afisa Afya na mazingira wa Manispaa ya Songea Dk.Vitalis Mkomela amesema manispaa ya Songea imepokea lita 1000 za dawa hiyo ambazo zimenunuliwa na Rais Dk.John Magufuli ambapo kiasi hicho cha dawa kinatosha kupulizia kipindi hiki cha kiangazi katika mitaa 95 ya manispaa hiyo.
Amesema kabla ya kuanza kazi ya kupulizia hivi sasa yanaandaliwa mafunzo na miongozo kwa wafanyakazi wa kujitolea 95,wenyeviti wa mitaa 95 na maafisa afya ambao watapewa kwanza elimu ili waweze kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo.
“Idara itanunua pampu 98 zitakazotumika katika zoezi hilo,pia inahitajika usafiri ili wafanyakazi waweze kuanza kazi mapema kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa tano kabla ya jua la utosi’’,anasema.
Hata hivyo amesema mazalia ya mbu yakipingua,mbu wa malaria pia watapungua na hatimaye ugonjwa wa malaria kupungua na kutokomezwa katika Manispaa ya Songea.
Ili kuhakikisha zoezi hilo linatoa matokeo makubwa Dk.Mkomela amesisitiza kuwa kila dimbwi lenye mazalia litapuliziwa mara nne kwa mwezi sawa na kupulizia mfululizo kila baada ya siku saba na kwamba watapulizia mazalio ya mbu yaliyofunikwa na mazalio ya mbu yaliowazi.
Amesisitiza kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu ambapo katika kipindi cha masika manispaa itanunua dawa za kupulizia mazalio yote ambayo yatakuwepo katika kipindi hicho ili kuhakikisha kuwa mazalia ya mbu yanatokomezwa katika manipaa hiyo.
Jumla ya watu 133 katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea wamefariki dunia mwaka 2015 baada ya kuugua ugonjwa wa malaria.Watanzania 60,000 wanakufa kila mwaka kutokana na ugonjwa wa malaria ambapo kila siku nchini watu 291 wanapoteza maisha kutokana na malaria.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa