RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Magufuli ametoa msaada wa shilingi milioni tano kwa Mwenye ulemavu wa viungo Konsaluva Lungu mkazi wa Mshangano Manispaa ya Songea.
Fedha hizo zimekabidhiwa kwa Konsaluva kwa niaba ya Rais na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme katika hafla iliyofanyika katika Benki ya CRDB tawi la Songea.
Mndeme amesema kitendo cha Rais kutoa msaada kwa mwenye ulemavu huyo kumedhihirisha kuwa ni Rais wa wanyonge na kwamba anawapenda watanzania na kuwajali.
Mndeme amesema Rais Magufuli baada ya kuona taarifa ya Konsaluva kwenye vyombo vya habari akifanyakazi kwa kujituma licha ya kuwa na ulemavu,aliguswa na kuamua kumsaidia.
“Mheshimiwa Rais anatambua kuna wenye ulemavu wapo wengi ndani ya nchi,lakini alipendezwa namna Konsaluva alivyokuwa mbunifu kwa kufanyakazi na kulea mtoto wake bila wasiwasi’’,alisema.
Ametoa wito kwa wenye ulemavu kuacha kutumia ulemavu kama kigezo cha kuombaomba,badala yake watumie ulemavu kama changamoto hivyo wafanye kazi kwa bidii.
Mndeme amesema fedha hizo zitumike kununua cherehani kwa kuwa Konsaluva amejifunza ufundi kushona katika Chuo cha VETA Songea na kwamba fedha hizo zinaweza pia kumsaidia katika mambo mengine ya kujikimu na uzalishajimali.
Licha ya fedha hizo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amesema serikali itampatia kiwanja na kumpatia kibanda bure cha kufanyia biashara ambako ataweka cherehani yake na kwamba amehamishwa toka na kupelekwa katika nyumba yenye mazingira rafiki yenye huduma za maji na umeme.
Konsaluva Lungu ni Mwenye ulemavu wa viungo tangu kuzaliwa akiwa na mguu mmoja,hana mikono na amewekewa mguu wa bandia, amemshukuru Rais kwa msaada huo na ameahidi kufanyakazi kwa bidii.
Konsaluva amevishukuru vyombo vya habari kwa kumuibua na kutangaza habari zake hali iliyosababisha Rais kumuona na kumsaidia na kwamba baada ya kupata msaada huo atajituma katika kufanyakazi.
“Namshukuru Mungu na Rais Magufuli kwa kuniona,ameniambia kwamba nimpende Mungu na kila kitu ninachokifanya nimtangulize Mungu, Nakuahidi Rais Magufuli nitafanya kadiri ulivyonielekeza’’,alisisitiza Konsaluva.
Naye Meneja wa CRDB tawi la Songea Efrasiana Mwanja akizungumza baada ya kufungua akaunti ya Konsaluva katika Benki hiyo,amempongeza Rais kwa moyo wa upendo kwa watanzania.
Sisi sote tulitamani baba zetu wote wawe na moyo kama wa mheshimiwa Rais Magufuli,sisi kama Benki ya CRDB tumemuona Konsaluva ana mtoto mdogo tunamfungulia akaunti ya Junior Jumbo ,tutaanza na shilingi 100,000’’,alisisitiza.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Juni 5,2019
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa