Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Tamasha la Mwezi wa Urithi linalotambulika kama Urithi Festival, "Celebrating Our Heritage" litakalozinduliwa rasmi kitaifa katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma Septemba 15, 2018
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga amesema lengo la Tamasha hilo ni kuenzi, kudumisha, kuburudisha na kujifunza masuala muhimu yanayohusu Urithi wa Mtanzania hususani tamaduni zetu, historia, malikale na maliasili.
Ameongeza kuwa Tamasha hilo litasaidia kukuza utalii wa ndani kwa kuongeza muda wa watalii wa kimataifa kukaa nchini kwa vile Tamasha hilo linafanyika katika kipindi ambacho watalii wengi wanatembelea Tanzania
Aidha, Naibu Waziri huyo ametaja mikoa sita pamoja na tarehe zake ambazo Tamasha hilo litafanyika kitaifa, kwa kuanza na jiji la Dodoma tamasha hilo litaanza kufanyika kuanzia Septemba 15 hadi tarehe 22 na kwa Zanzibar litafanyika Septemba 23 hadi 29.Pia, kwa upande wa Dar es Salaa na Mwanza tamasha hilo litafanyika Septemba 29 hadi Oktoba 6.
Aidha, kwa upande wa Wilaya ya Karatu tamasha hilo litafanyika kuanzia Oktoba 8 hadi 12, wakati kwa Jiji la Arusha tamasha hilo linatarajiwa kutafanyika Oktoba 8 hadi 13 mwaka huu.
Ameongeza kuwa Tamasha hilo litapambwa na shamrashamra za carnival ya mirindimo ya urithi, burudani za ngoma za asili, muziki na kwaya pamoja na sanaa za maonesho ya bidhaa ya wadau.Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo amesema tamasha hilo la urithi litanadiwa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kupitia themes za Mvalishe, Misosi ya Kwetu na Michongo ya Urithi.
Tamasha la Urithi Festival litakuwa linafanyika kila mwezi Septemba ya kila mwaka kuanzia mwaka huu.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa