Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amewataka wadau wa usafirishaji Mkoani Ruvuma kuzingatia muongozo uliotolewa na Wizara ya afya katika kukabiliana na wimbi la tatu la UVIKO 19.
Hayo yamebainishwa leo tarehe 05.08.2021 alipokutana na wadau wa usafirishaji pamoja na viongozi mbalimbali Mkoani Ruvuma katika ukumbi wa Manispaa ya Songea kwa lengo la kujadiliana namna ya kupunguza maambukizi ya UVIKO 19 katika Nyanja ya usafirishaji.
Ibuge ameagiza vyombo vyote vya usafiri kuhakikisha wanabeba abiria kulingana na idadi inayotakiwa pamoja na kunatumia vifaa kinga ikiwemo na vipukusa mikono ndoo za maji tiririka kwenye maeneo yote ya stendi na kuhamasisha uvaaji wa barakoa kwa abiria wote wanaotumia vyombo hivyo vya usafiri kama vile mabasi, daladala, bajaji na bodaboda.
Ameongeza kuwa viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea wanatakiwa kuweka misimamo ya msingi katika maeneo ya stendi ya Mfaranyaki, Ruhuwiko na Seedfarm ambazo zinatakiwa kutumika kwa ajili ya kushusha abiria na kuitaka stendi ya Shule ya Tanga itumike ipasavyo kwa kupakia na kushusha abiria jambo ambalo litapunguza msongamano wa watu na vilevile kuiendeleza stendi kuu ya mabasi Shule ya Tanga.”Alisisitiza”
Amewataka wakala wa barabara Ruvuma (TANROADS) kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa wa daraja la Bombambili kwa muda hadi kufikia Septemba 10, 2021 ili kuondoa adha ya usafiri kwa abiria na watumiaji wa barabara hiyo.
Pia amemtaka Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kwa kushilikiana na vyombo vya mawasiliano kuhakikisha anaweka mkakati wa kutoa elimu kwa umma kuhusiana na namna ya kujikinga na ugonjwa wa UVIKO 19 pamoja na umuhimu wa kupata chanjo ya ugonjwa huo kwa hiyari.”Alieleza”
Ibuge amewasisitiza wadau wote wa usafirishaji Mkoani Ruvuma kuzingatia na kutii sheria za barabarani ikiwemo na kufunga mikanda na endapo kutakuwa na ukiukwaji wa sheria hizo hatua kali zichukuliwe na mamlaka husika.
IMEANDALIWA NA,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA,
05.08.2021.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa