Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanal. Ahmed Abbas Ahmed leo amefanya ziara ya kushtukiza katika soko la Bombambili lililopo Manispaa ya Songea kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili wafanyabiashara wa soko hilo.
Katika ziara hiyo iliyofanyika tarhe 01 Agosti 2025, Kanal Ahmed aliwataka wananchi kutumia fursa wanapokutana na viongozi kutoa kero zao moja kwa moja ili zipatiwe majibu na ufafanuzi wa papo kwa papo, badala ya kunung’unika bila hatua kuchukuliwa.
“Niwapongeze kwa kazi mnayoifanya. Serikali ipo bega kwa bega nanyi, tunahitaji kujua changamoto zenu ili tuweze kuzitatua kwa wakati,” alisema Kanal Ahmed.
Baada ya kukagua mazingira ya soko na kusikiliza kero za wafanyabiashara, alibainisha changamoto mbalimbali ikiwemo uchafu wa mazingira, miundombinu ya barabara kuwa mibovu, na mlundikano wa wafanyabiashara bila mpangilio rasmi.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa alitoa maagizo kwa wataalamu wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kuhakikisha ndani ya siku 7 wanawapanga wafanyabiashara kwa utaratibu mzuri, na pia kuweka mikakati madhubuti ya usafi wa mazingira.
Aidha, alitoa agizo la kutekeleza zoezi la kuchonga barabara zinazozunguka soko hilo ndani ya siku 14, akisisitiza kuwa utekelezaji huo ni wa lazima kwa maendeleo ya eneo hilo la biashara.
“Usafi hauridhishi. Mlundikano wa wafanyabiashara unaonesha kutopangwa, kuna maeneo yameachwa wazi pasipo matumizi. Miundombinu ya barabara ni mibovu na kuna uchafu wa mazingira,” alifafanua Kanal Ahmed.
Kuhusu mikopo ya asilimia 10 kutoka Halmashauri, aliagiza wataalamu waendelee kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya jamii ikiwemo madereva wa bodaboda, bajaji, mama lishe na wajasiriamali wadogo ili waweze kunufaika.
Katika hatua nyingine, alitoa maagizo kwa Halmashauri kuhakikisha maduka yote yaliyofungwa kwa sababu ya kutolipa ushuru yafunguliwe, huku wakiweka utaratibu wa wafanyabiashara kulipa kwa awamu.
“Wale wote mliowafungia kwa sababu ya kudaiwa, wafungulieni maduka yao. Wekeni utaratibu wa kulipa kwa awamu hadi wakamilishe,” alisisitiza Mkuu wa Mkoa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Kapenjama Ndile alitoa wito kwa wananchi kudai utekelezaji wa miundombinu, akibainisha kuwa baadhi ya changamoto zinahitaji hatua zaidi ikiwemo uvunjaji wa nyumba na uondoshaji wa makaburi yaliyopo kwenye maeneo ya miundombinu, zoezi ambalo linakadiriwa kugharimu takriban Shilingi milioni 197.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa