Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
26 JUNI 2022
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali (Balozi) Wilbert Ibuge ameitaka Halmashauri ya Manispaa ya Songea kubuni vyanzo vipya vya mapato ili waweze kuwa na wigo mkubwa katika ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Ameyasema hayo leo wakati wa kikao cha Baraza maalum la Madiwani kupitia na kujadili taarifa ya mdhibiti mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
“Pamoja kupata hati safi ninatoa rai kwa Mkurugenzi mtendaji na timu ya wataalamu kuhakikisha mnaimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja na kuboresha matumizi ya fedha hizo lakini pia kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato” Alibainisha.
Brig. Ibuge amewataka viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kuhakikisha wanafunga hoja zote kufikia Juni 30 mwaka huu pamoja na kuzuiauwepo wa hoja za nyuma ambazo hujirudia mara kwa mara ambapo amesema wakuu wa Idara wote wanatakiwa kushiriki ipasavyo katika kuandaa majibu ya hoja na kufanyia kazi maelekezo ya CAG.
Aidha, amewataka Madiwani wote, kuhakikisha wanadhibiti mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali pamoja na kufuatilia suala la utoaji mikopo ya 10% kwa wanawake 4%, vijana 4%, na watu wenye ulemavu 2% na kufuata sheria na kanuni ili mikopo hiyo irejeshwe kwa wakati na kuwezesha wengine kunufaika na mikopo hiyo“Alisisitiza”
Ametoa rai kwa Madiwani kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa wananchi kwa kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kuchukua hatua za kinidhamu mapema kwa watumishi wasiotimiza wajibu wao kwa kufuata kanuni na misingi ya utawala bora.
Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema alianza kwa kuipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa kuweza kupata hati safi, hivyo amewataka wataalamu hao kuelekea mwisho wa mwaka wa fedha kila Halmashauri ihakikishe inapokea taarifa kutoka kwa mdhibiti mkuu wa hesabu za Serikali na kuzifanyia kazi kwa usahihi.
Kwa upande wake Mkaguzi Mkazi wa Mkoa wa Ruvuma Deogratius Waijaha amewataka viongozi kuhakikisha wanamalizia ujenzi wa bwalo la chakula katika shule ya Sekondari ya Emmanuel Nchimbi ili lianze kutumika pamoja na kufuatilia hati miliki ya viwanja vya masoko 7 na stendi 2 za mabasi.
Naye mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Hamisi Abdallah Ally amewataka Madiwani kuendelea kuunga mkono maono ya Serikali ya Awamu ya sita kwa kutimiza wajibu wao wa kuleta maendeleo kwa wananchi waliowachagua pamoja na kuhakikisha wanasimamia shughuli zote za maendeleo pamoja na usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani kuhakikisha unavuka malengo ya Halmashauri waliyojiwekea.
Akihitimisha Baraza hilo Mstahiki Meya Manispaa ya Songea Michael Mbano alibainisha kuwa kwa mujibu wa taarifa ya fedha iliyotolewa tarehe 31 Marchi 2022 makusanyo ya mapato ndani kwa Halmashauri tayari yamevuka lengo walilojiwekea kwa zaidi ya asilimia 100% pamoja na utoaji wa fedha asilimia 10% za mapato ya ndani kwa vikundi ambapo sh. Million 700 tayari zimeshatolewa.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa