TASAF ni chombo cha serikali kilichoundwa kwa lengo la kusaidia jitihada za wananchi katika kuondoa kero ya umaskini, kukuza uchumi na kuongeza kipato, kuboresha huduma za jamii na kuendeleza watoto wanaoishi kwenye kaya za walengwa katika sekta ya elimu, afya na lishe.
Ili kufanikisha Mipango hiyo, TASAF imefanya kikao kazi kwa wataalamu kwa lengo la kuwajengea uelewa juu ya utekelezaji wa kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya TASAF kinachofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea kuanzia 19-23 Aprili 2021 na kuhudhuriwa na Waheshimiwa Madiwani na Wataalamu na viongozi mbalimbali Manispaa ya Songea.
Mgeni rasmi katika mafunzo hayo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme ambaye katika hotuba yake ya ufunguzi wa kikao hicho alisema “ tathimini ya utekelezaji wa kipindi cha kwanza cha awamu ya tatu ya TASAF kinaonesha kuwa Mpango huu umechangia kwa kiasi kikubwa kufikia lengo la Serikali la kupunguza umaskini nchini kukiwa na takwimu zinazoonesha utekelezaji wa Mpango kwenye kipindi cha kwanza awamu ya tatu Mkoani Ruvuma wenye wanufaika 44,836.”
Mndeme ametoa wito kwa washiriki wote wa mafunzo hayo kufanya kazi kwa weredi ili kufanikisha kutekeleza Mpango wakuibua kaya lengwa ambapo alisema endapo atagundua kama kuna ongezeko la kaya hewa ambazo zitawekwa kwa upendeleo wowote hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao “alisema ukizingua tutazinguana”. ‘Alisisitiza’
Akitoa pongezi kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Tina Sekambo pamoja na timu ya wataalamu wa Manispaa ya Songea kwa kupata hati inayoridhisha. Hata hivyo ametoa rai kwa wafanyabiashara wote Mkoani Ruvuma kuhakikisha wanauza bidhaa zao kwa bei nafuu hasa katika msimu huu wa Ramadhani na endapo itabainika kuna mfanyabiashara yeyote amepandisha bei kwa maslahi binafsi hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Naye Kaimu Meneja wa mpango wa kukuza uchumi TASAF Catherine Kissanga alisema mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi cha kwanza ni asimilia 70% ya vijiji/mitaa/shehia zote nchini hivyo bado kuna wananchi wanaoishi katika hali duni kwenye maeneno ambayo hayakufikiwa.
Kisanga alisema Kipindi cha pili kilianza kwa uhakiki wa walengwa wote na kuondoa kaya zote za walengwa ambazo zimepoteza sifa mara baada ya kujitokeza kwa malalamiko mengi kuhusu Mpango kuwa na watu wasiostahili wakiwemo watu wasio maskini, viongozi, orodha ya watu waliohama au waliofariki ambao wote ni walengwa hewa.
Alisema kipindi cha pili cha awamu ya tatu TASAF ambacho kitatekelezwa katika halmashauri zote 184 za Tanzania Bara na Wilaya zote za Zanzibar, na kufikia kaya milioni moja laki nne na nusu zenye jumla ya watu milioni 7 nchini ikiwa ni nyongeza ya kaya laki tatu na nusu kutoka kwenye kipindi cha kwanza cha Mpango huo.
Kisanga alibainisha kuwa jumla ya kaya lengwa 4221 Manispaa ya Songea zimefikiwa na TASSAF ambapo Mpango huu utaendelea kusaidia kaya zenye hali duni kwenye vijiji, mitaa na shehia zote ambazo Mpango huu unawezesha kaya maskini hasa watoto wenye umri chini ya miaka mitano 5 ambao wanahudhiria kliniki, wanafunzi wanaosoma shule za awali, shule za msingi na shule za sekondari, akina mama wajawazito pamoja na kaya zenye ulemavu na uhakikisha wanapata lishe bora, huduma za afya na elimu.
Alibainsha kuwa ili kuwajengea uwezo Wawezeshaji watakaosimamia Mpango wa kipindi cha pili cha Awamu ya tatu TASAF watapatiwa mafunzo na kusaini viapo vya uadilifu na kisha watatakiwa kushiriki kwenye zoezi la uibuaji wa kaya lengwa katika vijiji/Mtaa/Shehia.
‘Kisanga alisisitiza’.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Michael Mbano amewataka Waheshimiwa Madiwani Manispaa ya Songea kuleta ushirikiano kwa wataalamu watakao shiriki katika kuibua kaya lengwa na kuhakikisha usimamizi wa Mpango wa TASAF wa kipindi cha pili unawafikia walengwa waliokusudiwa.
Nao washiriki wa mafunzo hayo wakitoa pongezi kwa Serikali kwa kuwawezesha mafunzo ambayo yatawasaidia kuwajengea uwezo wa kufahamu kuhusu namna ya kuibua kaya maskini katika kipindi cha pili Awamu ya tatu TASAF ambacho kinalenga kuongeza mitaa 36 mipya ambayo haikufikiwa kwenye kipindi cha kwanza Manispaa ya Songea.
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY;
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA.
20 APRILI 2021
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa