Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, ametoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Ruvuma kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi la kupiga kura litakalofanyika tarehe 29 Oktoba 2025, akisisitiza kuwa ni haki ya kikatiba na njia halali ya kuchagua viongozi wanaoaminiwa kuwa watawatumikia wananchi kwa uadilifu.
Amesema Serikali kupitia vyombo vyake vya usalama imejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa mazingira ya uchaguzi yanakuwa salama, tulivu na huru kwa kila mwananchi ambapo ameeleza kuwa ulinzi utaimarishwa katika maeneo yote ya kupigia kura ili kutoa fursa kwa kila mwananchi kushiriki katika mchakato huo wa kidemokrasia bila woga wala usumbufu wowote.
Aidha, RC Abbas ametoa onyo kali kwa mtu au kikundi chochote kitakachojaribu kuvuruga amani, kuchochea vurugu, au kufanya vitendo vya uvunjifu wa sheria, akibainisha kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wahusika kwa lengo la kudumisha amani, utulivu na usalama wa wananchi.
“Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa maeneo yanayojivunia kuwa na utulivu na mshikamano wa kijamii na amewataka kuilinda sifa hiyo kwa kushiriki uchaguzi kwa amani na utulivu kwa kuheshimu sheria na taratibu ziliyowekwa na Tume ya Uchaguzi,” alisema Brigedia Jenerali Abbas.
Akizungumza katika kikao cha amani kilichofanyika leo katika ukumbi wa Songea Club na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa amani, ambapo amewasihi wananchi Mkoani Ruvuma kutumia haki yao ya kupiga kura kwa amani ya nchi, akisisitiza kuwa endapo amani hiyo itatoweka, hakuna wa kuja kuiokoa.
Kwa upande wao, wadau wa amani na wananchi walioshiriki kikao hicho wameishukuru Serikali kwa juhudi zake za kuimarisha amani, huku wakiahidi kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi kwa utulivu na kuheshimu sheria.
Zoezi la kupiga kura linatarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, ikiwa ni siku 8 tu zilizobaki kabla ya siku hiyo muhimu kwa taifa.
MWISHO
Amina Pilly
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa