Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, amewapongeza Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa ushindi waliopata katika uchaguzi, akisisitiza kuwa ni heshima kubwa lakini pia ni wajibu mzito unaohitaji nidhamu, uadilifu na kujitolea kwa dhati katika kuwatumikia wananchi.
Pongezi hizo zilitolewa katika Mkutano wa Kwanzawa Baraza la Madiwani uliofanyika tarehe 2 Desemba 2025 katika ukumbi wa Manispaaya Songea, mkutano uliolenga kuunda baraza jipya, kutoa viapo kwa madiwani nakupokea taarifa ya utendaji ya Halmashauri kwa kipindi cha Julai 1 hadi Desemba1, 2025.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Mkoa aliwataka viongozi hao kushirikiana na wataalamu wa Halmashauri kusimamia ukusanyaji wa mapato, kuboresha vyanzo vilivyopo na kuhakikisha mifumo yaukusanyaji inakuwa thabiti na yenye uwazi. Pia aliwataka kuwa makini katika usimamizi wa miradi ya maendeleo na kuchukua hatua pindi wanapoona upotevu au matumizi mabaya ya fedha za serikali.
“Nendeni mkahakikishe watendaji wanaosimamia makusanyo wanafanya kazi kwa uadilifu.Mnapoona upotevu wa mapato, chukueni hatua bila kuchelewa. Hakikisheni pia watumishi wanapata stahiki zao ikiwemo mafao ya likizo na maslahi mengine,”alisisitiza Brigedia Jenerali Abbas.
Aidha, aliwahimiza madiwani kushughulikia changamoto za wananchi na kuendelea kushirikiana na serikali ya mkoa, watendaji wa Halmashauri na wadau wa maendeleo ili kuleta maendeleo ya kweli ndani yaManispaa ya Songea.
Katika hatua nyingine, Baraza la Madiwani lilifanya uchaguzi wa Meya na Naibu Meya, ambapo Katibu Tawala wa Wilaya ya Songea, Mtella Mwampamba, alitangaza matokeo ya kura 30 zilizopigwa bila kuharibika. Ndugu Abrahamu Egno Mbunda alichaguliwa kuwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea, huku Edith Chiwango akichaguliwa kuwa Naibu Meya kwa kura zote 30.
Akizungumza baada ya matokeo, Mwampamba alisema wananchi wanamatarajio makubwa kutoka kwa viongozi wao, hivyo ni muhimu kuongoza kwa weledi, kuheshimiana na kukosoana kwa ujenzi, ili kuepuka migogoro inayoweza kurudisha nyuma maendeleo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea, Wakili Bashir Muhoja, aliwasilisha taarifa ya utendaji akieleza kuwa hadi kufikia Desemba 1, 2025, Halmashauri imepokea na kutumia fedha kulingana na mpango na bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026. Kiasi cha shilingi bilioni 26.58 sawa na 101.2% ya makadirio kilipokelewa kwa matumizi ya kawaida, huku zaidi ya shilingi bilioni 26.03 zikitumika kugharamia shughuli mbalimbali. Aidha, mapato ya ndani yaliyokusanywa yalifikia shilingi bilioni 3.29 sawa na 53.8% ya makisio ya mwaka.
Kwa upande wa fedha za maendeleo, Halmashauri ilipokea shilingi bilioni 5.88 sawa na 42.04% ya makisio ya mwaka mzima.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Komredi Oddo Mwisho, aliwapongeza madiwani na wabunge kwa ushindi na kuwasisitiza kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa mapato, kutunga sheria rafiki kwa wananchi na kuweka mipango yenye tija kwa jamii.
Viongozi mbalimbali walisisitiza kuwa wataendelea kushirikiana na wataalamu na wananchi kuhakikisha maendeleo yanapatikana ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
Baraza hilo lilihudhuriwa na Viongozi ngazi ya Mkoa na Wilaya, viongozi wa vyama vya siasa. Wananchi na wadau mbalimbali.
NA;
Amina Pilly
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa