Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme ametoa agizo hilo leo katika kikao chake cha utatuzi wa Mgogoro baina ya mwekezaji wa ndani na mwekezaji wa nje wa Mgodi wa Makaa ya Mawe unaomilikiwa na Kampuni ya ( MIL-COAL Songea), kilichofanyika katika ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa tarehe 04/09/2020.
Mndeme alisema” awali alipokea mgogoro wa Wawekezaji wa Mgodi wa makaa ya mawe unaotambulika kwa jina la Market Insigut Limited (MIC-COAL Songea) ambapo aliunda tume ya Uchunguzi na hatimaye alibaini mapungufu ya kimkataba baina ya Mwekezaji wa ndani na mwekezaji wanje.
Alibainisha kuwa sambamba na changamoto iliyojitokeza tume hiyo imebaini uwepo wa baadhi ya mapungufu yanayoikabili kampuni hiyo ya Madini pamoja na Kampuni kutolipa kodi ya Serikali zaidi ya Tsh milioni 274, Kutolipa mishahara ya Watumishi kwa wakati, pamoja na upotevu wa fedha za malipo yamishahara ya wafanyakazi zaidi ya milioni 62 zilizochukuliwa na Fredrick Mwaipopo ambaye alikuwa mhandisi wa Kampuni hiyo.
Hata hivyo baada ya kutatua mgogoro huo, amewaagiza Wawekezaji hao kuanza kazi rasmi leo ya uchimbaji wa Makaa ya mawe, kulipa kodi wanayodaiwa Zaidi ya Milioni 274, kulipa madai yote ya Watumishi wanayodaiwa, kufungua ajira kwa Watanzania, kuuza makaa ya mawe kwenye viwanda vya ndani ili vipate nishati ya kutosha, na kulipa kodi ya huduma ( service leavy) ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.
Aidha, aliagiza kukamatwa kwa Fredrick Mwaipopo ( Mhandisi wa Kampuni) ambaye anatuhumiwa kuhujumu uendeshaji wa Mgodi kwa kuchukua fedha milioni 62 ambazo zilikuwa malipo yamishahara ya wafanyakazi wa Mgodi huo.
Naye Kaimu Afisa madini Mkoa wa Ruvuma Jumanne M. Nkana alisema” baada ya kupokea malalamiko ya wawekezaji hao aliwaita na kusuluhisha kwa kufanya mapitio ya mkataba wao wa awali ambao mwekezaji wa ndani alikuwa anapata 30% na mwekezaji wa nje alikuwa anapata 70%, hata hivyo mkataba huo ulirekebishwa kwa awamu nyingine na kukubaliana kuwa mwekezaji wa ndani atapata 37.5% na mwekezaji wa nje atapata 62.5% ambapo bado mgogoro uliendelea na hatimaye walishauriwa kutumia utaratibu wa mwingine ambao unatumika kila tani inayouzwa lazima ilipwe kiasi cha fedha.”
Jumanne aliongeza kuwa, Kampuni hiyo ilisimama kufanya kazi kwa muda mrefu kuanzia disemba 2019 na hii nikutokana na kuharibika kwa miundombinu ya barabara kuanzia eneo la mgodi hadi sehemu ya kuweka makaa ya mawe, na baada ya kubaini hilo ililazimu kutengeneza miundombinu na hatimaye mwezi aprili 2020 Kampuni hiyo ilianza kusafirisha makaa ya mawe kutoka mgodini.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Cosmas M. Nshenye alitoa ushauri kwa kampuni hiyo kuboresha vitendea kazi vya watumishi kama vile (Barakoa), kuboresha miundombinu, na malipo ya mishahara ya wafanyakazi.
IMETAYARISHWA NA;
AMINA PILLY;
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA.
04.09.2020
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa