“Uteuzi wa viongozi hawa unawataka kuja kusimamia malengo ya serikali kwa kuhakikisha wananchi wanaishi sehemu salama.”
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 22 juni na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Generali Wilbert Ibuge akiwa katika usimamizi wa zoezi la utoaji kiapo kwa Wakuu wa Wilaya ya Namtumbo Julius Keneth Ningu na Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Col. L.E. Thomas kilichofanyika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma na hudhuriwa na Makatibu Tawala Mkoa/ Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri 8, Wazee wa Kimila, Viongozi wa dini pamoja na kamati ya ulinzi na usalama.
Ibuge alisema Lengo la serikali ni kuhakikisha uwepo wa ulinzi na usalama katika maeneo yao kwa kuhakikisha wananchi wanakuwa salama pamoja na kuwashirikisha wenyewe katika suala la ulinzi shirikishi jamii kwa ajili ya maslahi yao binafsi na Nchi kwa ujumla.
Sambamba na uwajibikaji, amewataka viongozi hao kusimamia maendeleo ya kiuchumi na kijamii ikiwemo na usimamizi wa miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao na kuhakikisha inakuwa yenye tija, yenye thamani ya fedha ambayo imetengewa na kukamilishwa kwa kiwango kinachostahili. “ Ibuge alisisitiza”
Alibainisha kuwa, fedha zitokanazo na mapato ya ndani wahakikishe inatengwa asilimia 10 kwa ajili ya kuwezesha makundi maalumu “wanawake 4%, vijana 4% na walemavu 2%” pamoja kusimamia vizuri urejeshwaji wa fedha hizo ambazo hazina riba ili ziweze kuwasaidia wanavikundi wengine.
Aliongeza kuwa kila kiongozi katika maeneo yake ahakikishe anahamasisha wananchi juu ya kujiunga na huduma ya Bima ya Afya iliyoboreshwa CHF pamoja na kusimamia fedha zote zinazotakiwa kununuliwa dawa zinawekwa Benk na dawa ziombwe kupitia mifumo inayoeleweka.
Ibuge alisema Mkoa wa Ruvuma ni Mkoa adhimu ambao wananchi wake wanajituma nani Mkoa ambao hauna historia ya njaa kwani wananchi wenyewe hujizalishia chakula wenyewe na kujilisha. Hivyo amewataka wahakikishe wanasimamia mazao ya kimkakati na ya kibiashara ambayo ni muhimu kwa ajili ya kuongeza uzalishaji na kipato cha mtu mmoja mmoja.
Hata hivyo ametoa Rai kwa viongozi hao kuendelea kusimamia utekelezaji wa Sera kama zilivyoainishwa ikiwemo na utatuzi wa kero za wananchi, ambapo alisema endapo kero za wananchi zitaachwa na kukomaa zitafifisha maendeleo ya wananchi.
Amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu ambao husababisha kushindwa kupumua, ambapo alisema ni bora kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya kwani kinga ni bora kuliko tiba.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Julius Nungu alisema atafanyakazi kwa kushirikiana na wananchi na atategemea sana kujifunza kupitia kwao wananchi, ambapo alibainisha kuwa bila ya uwepo wa wao wananchi yeye si kiongozi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Col. L. E. Thomas alisema hahitaji kuwa kiongozi mtawala bali atakuwa mtumishi wa wananchi wa Nyasa na atachukua changamoto zilizopo na kuzibadili kuwa fursa.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dkt. Jairy Khanga alisema hatunabudi kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya wimbi la tatu la homa kali ya mapafu pia akiwataka wananchi kwa ujumla kuchukua tahadhari na kuepuka Mikusanyiko isiyoyalazima au kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka na kutumia vitakasa mikono.
Dkt. Khanga amegawa vipaza sauti kwa wakuu wa Wilaya kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya homa kali ya mapafu. Amewaondoa hofu wananchi Mkoani Ruvuma kuwa hadi hivi sasa Mkoa upo salama hakuna mgonjwa yeyote au mhisiwa bali tuchukue tahadhari.
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY;
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA.
22 JUNI 2021.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa