Serikali za mitaa ni chombo kilichoanzishwa kisheria kwa mujibu wa Ibara ya 145 na 146 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambayo imetaja majukumu ya Serikali za mitaa katika Halmashauri yakiwa yameainishwa katika sura ya 287.
Hayo yamebainika katika mkutano mkuu wa kwanza wa Uchaguzi wa Meya na Naibu Meya na wajumbe wa kamati za kudumu za Halmashauri ambapo kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji wa mkutano wa kwanza wa Halmashauri huongozwa na katibu tawala wa Wilaya.
Mkutano huo ulifunguliwa na Katibu Tawala Wilaya ya Songea Pendo Daniel uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa lengo la kuwapatia Madiwani hao tamko la maandishi, kumchagua Meya na Naibu Meya, kuunda kamati za kudumu za Halmashauri, kupokea taarifa mbalimbali za utekelezaji wa shughuli za Halmashauri zilizofanyika katika kipindi ambacho baraza la madiwani lilivunjwa pamoja na kiapo cha uadilifu.
Awali Madiwani hao walitoa Tamko la maandishi na kiapo cha uadilifu kilichotolewa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea Livini B. Lyakinana.
Pendo Katika hotuba yake ya ufunguzi iliyosomwa mkutanoni hapo nanukuu” shughuli na maamuzi katika serikali za mitaa hufanywa kupitia mikutano na vikao ambavyo huongozwa kwa kanuni za kudumu zilizoizinishwa na Waziri mwenye dhamana za Serikali za mitaa ikiwa imekataza kutokuwepo kwa migogoro na migongano miongoni mwa madiwani wenyewe na watendaji wa mamlaka.” Mwisho wa kunukuu.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi baada ya zoezi la upigaji kura wa kumchagua Meya na Naibu Meya ambapo Michael Leodgar Mbano alipata kura 28, kura zilizoharibika (hakuna), kura zilizokataliwa (hakuna), kura za ndiyo ni 28, hatimaye ndugu Michael L. Mbano alitangazwa kuwa Meya wa Manispaa ya Songea. Hatua ya pili ilikuwa ya kumchagua Naibu Meya ambapo kura zilizoharibika (hakuna), kura zilizokataliwa (hakuna), kura za ndiyo ni 28 na hatimaye ndugu Jeremia Green Mlembe kutangazwa kuwa Naibu Meya Manispaa ya Songea.” Pendo alitamka.”
Baada ya kutangazwa kwa matokeo ya ushindi wa nafasi ya Meya na Naibu Meya kwa pamoja viongozi hao walitoa shukrani kwa chama cha mapinduzi kwa kuwateua kugombea nafasi hizo walizozipata wakisisitiza kufanya kazi kwa kushirikiana baina ya Madiwani wenzao, wananchi waliowachagua pamoja na wataalamu kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia kanuni, miongozo, na taratibu zilizowekwa na Serikali.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme akihutubia baraza hilo kwa mara ya kwanza alilipongeza baraza lililomaliza muda wake 2019-2020 kuwa walifanya kazi nzuri ya kukusanya mapato na kufikia 99%, amewaasa Madiwani hao kuongeza jitihada za ukusanyaji wa mapato kuanzia 99% hadi 100% ifikapo june 2020-2021.
Mndeme amewataka madiwani hao kusimamia kituo kipya cha mabasi cha Tanga kuanza kufanya kazi ifikapo 31 disemba 2020, Machinjio mpya ya Tanga ianze kufanya kazi kabla ya tarehe 1 Januari 2021, kuhamasisha wafanyabiashara kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa letu, kufungua kiwanda kipya cha utengenezaji wa bidhaa za ngozi, pamoja na ujenzi wa hospitali ya Rufaa Mkoa wa Ruvuma.
Alisema haoni sababu ya msingi ya kutofanya kazi kituo kipya cha mabasi cha Tanga kukiwa kuna eneo la kupaki daladala, eneo la kupaki bodaboda na bajaji , eneo la kupaki tax, “ pamoja na uwepo wa vibanda 30 vya wafanyabiashara, vibanda 20 vya kukatia tiketi, na huduma ya bafu na vyoo ambayo hupatikana kituoni hapo. “ Alisisitiza”
Mwisho, amewaasa wajumbe wa kamati ya fedha kusimamia miradi ipasavyo ikiwemo na ufungaji wa mashine ya machinjio ya nyama ili iweze kuongeza ajira kwa kwa jamii.
IMETAYARISHWA NA;
AMINA PILLY;
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA.
16 Disemba 2020.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa