Mkoa wa Ruvuma umeungana na jamii ya kimataifa kuadhimisha kilele cha Siku ya Kimataifa ya Wazee, katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Songea Club, huku maadhimisho hayo yakiongozwa na kaulimbiu isemayo:
“Ushiriki wa Wazee katika Uchaguzi Mkuu kwa Ustawi wa Jamii.”
Lengo kuu la maadhimisho haya lilikuwa ni kutambua mchango mkubwa wa wazee katika maendeleo ya taifa, pamoja na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika michakato ya kidemokrasia, hasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wadau wa maendeleo, na wananchi kutoka mikoa mbalimbali.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abas Ahmed, ambaye alikuwa mgeni rasmi, alitoa shukrani kwa wizara, washiriki, na waandaaji kwa kufanikisha maadhimisho hayo kwa mafanikio makubwa. Alisisitiza kuwa:
"Serikali ina jukumu la kuendeleza amani na kudumisha ustawi wa taifa kwa maendeleo endelevu. Wazee wanapaswa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi kwa kuwa ni haki yao ya msingi na njia ya kuchangia ustawi wa jamii."
Aliongeza kuwa jamii inapaswa kuendelea kujenga uelewa na kutoa hamasa kuhusu haki na maslahi ya wazee nchini.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju, aliipongeza wizara ya afya kwa kuratibu utoaji wa huduma za afya kwa wazee. Pia alisisitiza kuwa serikali inaendelea kuimarisha huduma za kijamii kwa wazee kwa kuhakikisha Ushirikishwaji wao katika sera, miongozo na mipango ya maendeleo,Wazee wanapata huduma stahiki za kijamii pamoja na Vijana wanahamasishwa kuwaheshimu na kuwatunza wazee kama sehemu ya kudumisha maadili ya taifa
Naye Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mheshimiwa Kapenjama Ndile, aliwashukuru wageni kutoka mikoa mingine kwa kushiriki maadhimisho hayo, na kuwataka waendelee kushirikiana kwa karibu katika kuwaenzi wazee.
“Tunawashukuru kwa kuungana nasi katika siku hii muhimu ya kitaifa, ambayo inaleta mshikamano na kutambua nafasi ya wazee katika jamii yetu,” alisema.
Maadhimisho haya yameonesha dhamira ya dhati ya serikali na wadau wa maendeleo katika kulinda haki, heshima na ustawi wa wazee, sambamba na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika masuala ya kijamii na kisiasa, ikiwa ni pamoja na uchaguzi mkuu ujao
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa