MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme ameagiza hadi kufikia Septemba 30 mwaka huu vikundi vyote ambavyo bado havijalipa mikopo Yao waliochukua kupitia Benki za CRDB na TPB tawi la Songea wachukuliwe hatua za kisheria.
Akizungumza kwenye kikao cha ufuatuliaji wa madeni kilichofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea,Mndeme amesema Baraza la Taifa la Uwezesheji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Linadai vikundi,vyama vya ushirika na SACCOS zaidi ya shilingi milioni 197 ambazo walikopeshwa kupitia CRDB na TBP mkoa wa Ruvuma.
Kwa upande wake Meneja Mawasiliano wa CRDB Stephen Msigwa amesema hadi sasa Benki hiyo inadai jumla ya shilingi milioni 94 kati ya zaidi ya milioni 300 ambazo walivikopesha vikundi vya ujasirimali,vyama vya ushirika na SACCOS na kwamba wanatakiwa kulipa madeni yao ili waweze kutoa mikopo hiyo kwa watanzania wengine wanaohitaji kukopa.
Naye Meneja wa Benki ya Posta Mkoa wa Ruvuma Robert Kombo amesema benki bado inadai shilingi milioni 103 ambazo bado hazijalipwa na wajasirimali hao licha ya kwamba muda wa kulipa umemalizika.
Katika kikao hicho kimeundwa kikosi kazi cha watu sita cha ufuatiliaji wa madeni hayo akiwemo Mwakilishi wa Kamanda wa Mkoa wa Ruvuma lengo likiwa ni kuhakikisha madeni hayo yanalipwa ndani ya kipindi cha mwezi mmoja na kwamba hadi kufikia Septemba 30 deni lote liwe limelipwa na pasiwepo na mtu au kikundi ambacho hakijalipa.
Imeandikwa na Albano Midelo
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa