SELOUS: PORI LA KWANZA BARANI AFRIKA
Pori la Akiba la Selous lilianzishwa mwaka 1896 na Wajerumani likiwa pori la kwanza kutengwa kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori barani Afrika na la pili kwa ukubwa duniani baada ya pori la Marekani ambalo linaitwa Yellowstone National Park. Historia inaonesha kuwa jina la Selous limetokana na askari ambaye alikuwa ni mvumbuzi wa kiingereza aliyeitwa kapteni Fredrick Selous aliyefariki Januari 4, mwaka 1917 na kuzikwa katika eneo la Behobeho lililopo ndani ya pori la Selous .
kwa mujibu wa Meneja wa Pori la Akiba la Selous Mhifadhi Henock Msocha pori hilo lina ukubwa wa ukubwa wa kilometa za mraba 50,000 na linapita katika mikoa ya Ruvuma, Lindi,Pwani na Morogoro na wilaya ambazo zinapita katika Pori hilo ni Liwale, Kilwa, Rufiji, Kilombero, Morogoro vijijini, Malinyi, Namtumbo, Tunduru na Kisarawe
Pori la Akiba Selous lina utajiri wa viumbe adimu katika sura ya dunia kama vile nyani aina ya sanje,mbega mwekundu,faru mweusi ambaye yupo hatarini kutoweka na wanyama wengine wakiwemo ndege,wadudu na mimea ambayo haipatikani sehemu nyingine yeyote duniani. Kutokana na umuhimu wa pori la Selous Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Utamaduni na Sayansi (UNESCO) limelihorodhesha pori hilo kuwa ni moja ya maeneo ya asili ya urithi wa dunia tangu mwaka 1982.
Afisa Maliasili na Utalii wa Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe anasema Pori la Selous lenye idadi kubwa ya tembo ni mapito ya wanyama yaani ushoroba wa tembo ambao wanatoka katika pori hilo kupitia pori la Akiba la Liparamba na kuingia hifadhi ya Niassa nchini Msumbiji.
Takwimu zinaonesha kuwa katika pori hilo hadi kufikia mwaka 2007 kulikuwa na tembo zaidi ya 70,000 hata hivyo idadi ya tembo katika pori hilo ilishuka kutokana na kukithiri kwa ujangili hadi kufikia tembo 43,000 mwaka 2009 ambapo hivi sasa idadi ya tembo katika pori hilo inaongezeka kwa kasi baada ya serikali kuwadhibiti majangili.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa