Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amesema kwamba Serikali ya awamu ya tano kuanzia sasa haitabomoa tena nyumba za wananchi waliojenga maeneo ya makazi yasiyo rasmi badala yake itarasimisha makazi holela.
Waziri Lukuvi amesema Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ametoa fursa kwa wananchi wote masikini waishio mijini waliojenga bila ya kufuata mipango miji na hawana hatimiliki za ardhi kufanyiwa urasimishaji wa makazi yao na wasibomolewe nyumba zao tena kwakuwa haikuwa ni makosa yao kujenga maeneo hayo.
Lukuvi ameyasema hayo alipokuwa wilayani Simanjiro mkoa wa Manyara alipofanya ziara yake ya kusikiliza na kutatua migogoro ya ardhi kwa wakazi wa mji huo, ambapo amesema wananchi wote wachangamkie fursa hii iliyotolewa na Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ya kuwapa fursa ya kumiliki hati katika maeneo ambayo siyo rasmi kwa kurasimishiwa.
“Serikali ya awamu ya tano inajali sana wananchi wake kwakuwa zamani wananchi ambao hawakujenga kwa kufuata mipango miji wangebomolewa nyumba zao, lakini kwa sasa Serikali ya awamu ya tano imeanzisha mpango kurasimisha makazi holela na kuwapatia hati wananchi wote waishio mijini ili waishi katika makazi rasmi” Amesema Lukuvi.
Aidha, Lukuvi amewataka wananchi wote waishio mijini kuwa wazalendo kwa kurasimisha maeneo yao waweze kujipatia hati na ili walipe kodi ya pango la ardhi jambo ambalo litaiongezea Serikali mapato.
Lukuvi alipokuwa ziarani Simanjiro mwishoni mwa wiki aligundua kuwa wakazi wa mji wa Simanjiro wanalio na hatimiliki za ardhi hawazidi 1,000 wakati nyumba zilizopo ni nyingi zaidi ya idadi hiyo. Hivyo Waziri Lukuvi akawataka wachangamkie fursa hii ya kujipatia hati ili kuzipa hadhi nyumba zao.
“Nyumba isiyokuwa na hati haina thamani kwakuwa hata ukienda Benki kukopa pesa hawatakuuliza umejenga nyumba ya uzuri gani, lakini watakachotaka ni hati yako ya kumiliki ardhi ambacho ndio kitu kilicho na thamani zaidi kwako kuwa nacho” aliongeza Lukuvi.
Naye Mbunge wa Simanjiro Mheshimiwa James Ole Millya ambaye amehamia CCM akitokea Chadema amemshukuru Mhe. Lukuvi pamoja na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuwajali wananchi wake kwa kuwaletea maendeleo makubwa na kusimamia suala la wananchi wa kawaida kupata fursa ya kumiliki ardhi kutoka kwa wawekezaji wakubwa ambao walikuwa hawayaendelezi mashamba yao kwa muda mrefu.
Simanjiro ndio wilaya inayoongoza kwa wamiliki wa mashamba makubwa walio na hati na hata wengine wasio na hati rasmi. Kwa sasa mashamba makubwa yaliyo na hati rasmi yanafika 158 yaliyo na jumla ya hekari zaidi ya 120,000 ambapo wasio na hati ni zaidi ya hao, hivyo Waziri amenza utaratibu wa kufuta mashamba makubwa 55 wilayani humo yanayomilikiwa kwa kuwa wamiliki wake wamekiuka masharti ya umiliki.
|
|
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa