WAZIRI wa maji Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali itahakikisha miradi yote ya maji vijijini na mijini inakamilika kwa wakati ili kuwaondolea kero ya maji Safi na Salama wananchi ili waweze kufanya kazi kwa bidii za kujiletea maendeleo.
Aliyasema hayo hivi karibuni alipofanya ziara ya siku mbili ya kukagua miradi ya maji katika katika kijiji cha Ukuli Kata ya kingerikiti na kata ya Tingi.
Profesa Mbarawa alifafanua kuwa aliamua kufanya ziara ya kukagua miradi hiyo ya maji ili aione kwa macho na siyo kusubiri kuletewa kwa maandishi ili azijue changamoto gani zilizopo katika miradi hiyo ili aweze kuitatua na kuhakikisha Wananchi wanapata maji safi na Salama ikiwa ndilo lengo kuu la Serikali.
Aliongeza kuwa kwa muda mrefu alisikia kuna tatizo la maji katika kata ya Tingi na Kingerikiti hivyo akaamua aje aone,na kutolea ufafanuzi wa kuwa katika mradi wa Ukuli kuna tatizo la kupasuka kwa viungio vya kwenye bomba kutokana na bomba kupita kwenye miteremko mikali ikitokea kijiji cha burma na kuvuka hadi kijiji cha Ukuli na akasema ameona na ameliona tatizo ambalo atatuma wataalam kutoka Wizara yake ili waweze kutatua tatizo hilo na maji yaweze kutoka na wananchi wafurahie huduma ya maji safi na salama kwa kuwa serikali ilishatoa tsh 1,129,433,944.00.kwa ajili ya kutekeleza mradi wa Ukuli-Kingerikiti.
“nimefanya ziara ya siku mbili kuja katika kijiji hiki kwa lengo la kutatua tatizo lilopo katika eneo hili badala ya kukaa ofisini na kusubiri kuletewa tatizo kwa maandishi lakini leo nimefurahi nimekagua na niko huku kwenye hii miteremko ambayo nimefanikiwa kuona tatizo lililopo na nitatuma wataalam kuja kurekebisha bomba viungio hivi ambavyo vinapasuka tujue tatizo kubwa ni nini kwa kutumia fedha kidogo na kwa haraka tuweze kutatua tatizo lililopo na hatimaye wanachi waweze kupata maji safi na salama kwa kuwa mapendekezo niliyopata awali ni kupitisha mabomba haya sehemu nyingine”
Wakazi wa kijiji cha Ukuli kata yakingerikiti wakiongelea tatizo la maji katika kijiji hicho wanatumia umbali mrefu wa kilomita tatu hadi tano kutafuta huduma ya maji hivyo serikali ikifaulu kukamilisha mradi huo itakuwa imewapunguzia kero nzito ya upatikanaji wa maji katika eneo hilo.
Awali akitoa taarifa ya kero ya maji katika eneo hilo kwa Waziri wa maji kwa niaba ya wananchi wa kata ya Kingerikiti Diwani wa kata ya Kingerikiti Alto Komba ambaye pia ni mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa alisema Tatizo hilo ni kubwa linalowafanya wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji safi na salama.
Aidha alitumia fursa hiyo kuziagiza Halmashauri Nchini kusimamia vizuri miradi ya maji kuanzia kutangaza zabuni na kuwateua wakandarasi wenye sifa na uwezo wa kifedha ili waweze kukamilisha miradi kwa wakati na kutanguliza maslahi ya wanachi bila kujali maslahi yao binafsi.
Katika kijiji cha Tingi alikagua mradi wa maji wenye thamani ya tsh 361,233,107/= na kuwataka wanachi kuwa na subira wakati mradi huo unakamilishwa na kuwaahidi Serikali itahakikisha inachukua hatua ya kuwaleta wataalam na kuongeza chanzo kingine cha maji ili upatikanaji wa maji safi na salama uwe asilimia 85 kwa vijijini na mjini iwa aslimia 90 ifikapo mwaka 2020.
Aidha Waziri Mbarawa alitoa wito kwa jamii ya watanzania kuvilinda na kuvitunza vyanzo vya maji kwa kuacha kulima kwenye vyanzo vya maji na kuacha kukata miti ovyo ili maliasili iliyopo kwenye vyanzo vya maji viendelee kutoa maji kwa wakazi wa maeneo yote nchini.
Miradi hiyo ya maji itahudumia watu 6286 kwa kata ya kingerikiti na watu 7326 kwa kata ya tingi kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.
IMEANDALIWA NA
NETHO C. SICHALI
AFISA HABARI
NYASA DC
0783662568/0767417597
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa