Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
6 JULAI 2022
Serikali imejipanga kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi wa umma Mkoani Ruvuma.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala bora, Mheshimiwa Jenista Mhagama (Mb) aliyefanya ziara ya kutembelea Halmashauri ya Manispaa ya Songea leo tarehe 6 Julai 2022 kwa lengo la kutambua kero zinazowakabili watumishi wa umma pamoja na kukagua utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF).
Akizungumza na watumishi wa Manispaa ya Songea, Mhe. Mhagama amewataka Maafisa rasilimali watu wa Mkoa pamoja na Manispaa ya Songea kuhakikisha wanatatua changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi wa umma kabla ya kuzifikisha Wizarani.
Amewasisitiza Maafisa utumishi hao kutekeleza majukumu yao ikiwemo na kusimamia nidhamu na uwajibikaji wa watumishi wa umma kwa kufuata kanuni na taratibu za utawala bora.
Mhe. Mhagama ametoa rai kwa watumishi wa umma kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma kwa lengo la kuleta maendeleo kwa wananchi ambapo Serikali imeendelea kuboresha maslahi ya watumishi kwa kuongeza mishahara pamoja na posho za safari kuanzia mwaka mpya wa fedha 2022/2023.
Aliongeza kuwa Serikali imejipanga kuboresha mfumo wa ajira nchini ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ajira mpya elfu thelathini zinatarajiwa kutolewa pamoja na kupandisha vyeo na madaraja kwa watumishi zaidi ya Laki moja pia, watumishi elfu nane na themanini waliokidhi vigezo watabadilishwa vyeo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Pololet Kamando Mgema Mkuu wa Wilaya ya Songea amewataka watumishi wa umma kutimiza wajibu wao kwa kuongeza ufanisi katika utendaji kazi pamoja na kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya 6 za kuleta maendeleo nchini.
Pololet alisema kuwa Mkoa wa Ruvuma una upungufu wa watumishi elfu 80238 katika idara mbalimbali ambapo hadi sasa jumla ya watumishi wa umma walioajiriwa katika ofisi ya Mkoa ni elfu kumi na tatu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Dkt. Frederick Sagamiko alisema kuwa Manispaa ya Songea imetekeleza shughuli mbalimbali kwa mujibu wa muongozo wa utumishi wa umma kwa kusimamia zoezi la upandishaji madaraja kwa watumishi pamoja na kubadilisha vyeo (muundo) kwa watumishi 92 waliojiendeleza.
Akibainisha utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF) kwa Manispaa ya Songea, Dkt Sagamiko alisema kuwa katika kipindi cha Julai 2021 hadi Juni 2022 Manispaa ya Songea ilipokea jumla ya shilingi Bilioni 1.3 kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini kwa awamu ya pili ambapo jumla ya kaya elfu 5639 zinanufaika na mpango huo.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa