SERIKALI imetoa shilingi milioni 400 kwa ajili ya kujenga kituo cha Afya Kata ya Ruvuma Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma katika mwaka wa fedha 2017/2018.
Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Dk. Mameritha Basike amesema hadi sasa shughuli za ujenzi wa kituo hicho zinaendelea na ujenzi umefikia hatua ya msingi na kwamba mradi huo wa miezi sita unatarajia kukamilika Novemba 2018.
“Halmashauri imeendelea kutekeleza ujenzi mbalimbali katika sekta ya Afya, ambapo kwa sasa kuna ujenzi wa kituo kimoja cha Afya na Zahanati nane’’,anasisitiza Dk. Mamelitha Basike.
Hata hivyo licha ya changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya Afya, Halmashauri hiyo imefanikiwa kupunguza maambukizi ya UKIMWI kutoka asilimia 3.9 mwaka 2017 hadi kufikia 3.2 Machi 2018.
Amesema hali ya utoaji chanjo katika manispaa hiyo ni nzuri kwa sababu chanjo ya Penta tatu ambayo ndio kigezo cha mpango chanjo kitaifa imefikia asilimia 94, zaidi ya lengo la kitaifa la asilimia 90.
Dkt.Basike pia amezungumza suala la ongezeko la vifo vya wajawazito katika Manispaa hiyo bado ni tatizo na kwamba jitihada za kupunguza vifo hivyo zinaendelea.
“Vifo vya wajawazito/wazazi bado ni tatizo katika Halmashauri yetu kwani vifo hivyo vimeongezeka toka 182/10000 mwaka 2016 hadi 202/10000 mwaka 2017. Bado jitihada za kupunguza vifo hivyo vya wakina mama zinaendelea ikiwa ni pamoja na kuimarisha huduma za upasuaji katika kituo chetu” alisema Dkt.Basike.
Halmashauri ya Manispaa ya Songea imekua ikipokea dawa na vifaa tiba kutoka Serikali kuu kwa asilimia 91.1 hadi sasa. Hata hivvo Halmashauri hununua dawa za nyongeza kufidia zile zinazokosekana MSD kupitia vyanzo vingine vya fedha ikiwemo mfuko wa pamoja wa afya, Bima ya Afya, CHF pamoja na fedha za papo kwa papo.
Imetolewa na
Victoria Ndejembi,
Kitengo TEHAMA Manispaa Songea,
Agosti 21,2018.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa