Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Wakili. Bashir Muhoja, amezitaka idara zote zinazohusika na huduma za jamii kushirikiana kikamilifu na Idara ya Afya kupitia kitengo cha lishe ili kuhakikisha utekelezaji wa masuala ya lishe unafanyika kwa ufanisi zaidi katika jamii.
Akizungumza wakati wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa shughuli za lishe katika manispaa hiyo, Mkurugenzi huyo alisisitiza kuwa elimu ya lishe ni silaha muhimu katika kupunguza changamoto ya watoto kuzaliwa na uzito pungufu wa chini ya kilo 2.5, hali inayochangiwa kwa kiasi kikubwa na mimba za utotoni.
"Idara ya Afya inapaswa kusimamia kwa karibu utekelezaji wa afua za lishe, huku ikishirikiana kwa karibu na idara ya elimu, maendeleo ya jamii, ustawi wa jamii, kilimo na fedha ili kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara ya mimba za utotoni na umuhimu wa lishe bora," alisisitiza Mkurugenzi.
Aidha, alielekeza kuwa kila shule ya msingi na sekondari ndani ya Manispaa iwe na bustani ya mboga mboga zitakazohusishwa na vilabu vya lishe kwa lengo la kuwahamasisha watoto kujifunza na kupata lishe bora wakiwa shuleni.
Kwa upande wake, Afisa Lishe wa Manispaa hiyo, Bw. Robert Sinkamba, alisema kuwa uanzishaji wa vilabu vya lishe unaendelea kwa mafanikio makubwa, ambapo hadi sasa vilabu hivyo vimeanzishwa katika shule za msingi na sekondari kwa 72% wanafunzi kupata chakula shuleni.
“Tumekuwa tukitumia njia ya uhamasishaji kuanzisha vilabu vya lishe mashuleni, na zoezi hili limefanyika kwa mafanikio makubwa. Vilabu hivi si tu vinaelimisha kuhusu lishe, bali pia vimekuwa kichocheo kikubwa cha uzalishaji wa bustani za mboga,” alisema Simkamba.
Naye Kaimu Mweka Hazina wa Manispaa ya Songea, Elliassa Urrasa, alisema kuwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Manispaa hiyo imetumia asilimia 100 ya bajeti iliyotengwa kwa ajili ya lishe. Aliongeza kuwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Manispaa imetenga kiasi cha shilingi milioni 80 kwa ajili ya kuendeleza na kuimarisha shughuli za lishe katika jamii.
Mikakati hii inalenga kuhakikisha kuwa jamii ya Songea inakuwa na uelewa sahihi kuhusu lishe bora na umuhimu wake katika afya ya watoto, pamoja na kupunguza athari za mimba za utotoni zinazoathiri ukuaji na afya ya watoto wachanga
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa