Na Amina Pilly.
Watumishi wa Manispaa ya Songea wameibuka na ushindi katika mechi ya kirafiki dhidi ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma. Michezo hiyo ya kirafiki ilifanyika tarehe 23 Julai 2025 katika Uwanja wa Shule ya Msingi Namtumbo, ikijumuisha michezo ya mpira wa miguu, mpira wa pete na mpira wa wavu.
Katika mchezo wa mpira wa miguu, timu ya Manispaa ya Songea ilionesha ubora kwa kuifunga timu ya Namtumbo mabao 2 kwa 1. Vilevile, kwenye mchezo wa mpira wa pete, Songea waliendelea kung’ara kwa ushindi wa goli 32 dhidi ya 16 ya Namtumbo.
Hata hivyo, katika mchezo wa mpira wa wavu, watumishi wa Halmashauri ya Namtumbo walijibu mapigo kwa ushindi wa seti 2 kwa 1 dhidi ya Manispaa ya Songea.
Wakizungumza baada ya michezo hiyo, mmoja wa wawakilishi wa watumishi wa Manispaa ya Songea alieleza shukrani kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Wakili. Bashir Muhoja kwa kuruhusu watumishi kushiriki katika michezo hiyo, ambayo ni sehemu ya maandalizi kuelekea mashindano ya SHIMISEMITA (Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Serikali za Mitaa).
Michezo hiyo imetajwa kuwa ni fursa ya kuimarisha mahusiano ya kikazi, kuimarisha afya pamoja na kuongeza morali kwa watumishi katika utendaji wao wa kila siku.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa