Dawati la Huduma ya Ustawi wa Jamii katika Manispaa ya Songea limeandaa kikao kazi kilichowakutanisha viongozi mbalimbali wa serikali na wadau wa maendeleo, kwa ajili ya kufanya mapitio ya utekelezaji wa mradi wa utoaji huduma kwa watoto wa mitaani. Kikao hicho kimefanyika tarehe 17 Septemba 2025 katika ukumbi wa Songea Club.
Akizungumza katika kikao hicho, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Ruvuma, Bi. Mariam Juma, alieleza kuwa mwongozo wa kitaifa wa utoaji huduma za ustawi wa jamii unazitaka halmashauri zote nchini kuwa na ofisi maalum katika maeneo ya stendi za mabasi ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa walengwa, hususan watoto wa mitaani. Aidha, alibainisha kuwa shirika lisilo la kiserikali la Railway Children Africa limejitolea kufadhili mradi huo kwa kipindi cha mwaka mmoja, kuanzia Aprili 2025 hadi Machi 2026.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Railway Children Africa, Bw. Kidaha Mohamed, alieleza kuwa utekelezaji wa mradi huo tayari umeanza rasmi katika Stendi Kuu ya Mabasi Songea (eneo la Shule ya Tanga), ambapo shughuli za kupokea na kufanya utambuzi wa watoto wa mitaani zinaendelea. Alisisitiza kuwa mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali wa maendeleo kwa lengo la kutoa elimu kwa walezi wa hiari (free persons), pamoja na kufanikisha utambuzi wa watoto walioko mitaani katika maeneo yote ya Manispaa ya Songea.
Bw. Kidaha alihitimisha kwa kutoa wito kwa wadau wote kuendelea kushirikiana kwa karibu na mradi huo, hasa katika kuhakikisha huduma bora zinawafikia watoto walioko kwenye mazingira hatarishi.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Songea, Bi. Devotha Ndunguru, aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa dawati la huduma kwa watoto wa mitaani, ambapo hadi kufikia Septemba 2025, jumla ya watoto 19 walikuwa wametambuliwa — wavulana 11 na wasichana 8.
Bi. Devotha alitoa wito kwa wadau mbalimbali, wakiwemo LATRA, madereva wa bodaboda na bajaji, maafisa wa usalama barabarani (Traffic Police), wenyeviti wa mitaa, watendaji wa kata pamoja na wananchi kwa ujumla, kuendelea kutoa ushirikiano katika kufanikisha malengo ya mradi huo, kwa ajili ya ustawi na haki za watoto wa mitaani ndani ya Manispaa ya Songea.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa