Mtumishi wa Mungu, Nabii Suguye, ametembelea vituo vya kulelea watoto yatima katika Wilaya ya Songea kwa lengo la kuwafariji na kuwapatia misaada ya mahitaji muhimu.
Ziara hiyo iliyofanyika tarehe 25 Septemba 2025, ilihusisha vituo vitatu ambavyo ni St. Anthony, St. Teresia na SWACO, ambapo Nabii Suguye alikutana na watoto pamoja na walezi na walimu wao. Katika ziara hiyo, alikabidhi msaada wa chakula, sabuni, mafuta ya kupaka na kutoa ujumbe wa matumaini na upendo kwa watoto hao.
Akizungumza katika ziara hiyo, Nabii Suguye aliwapongeza waandishi wa habari kwa mchango wao mkubwa katika maendeleo ya taifa na kueleza kuwa lengo la ujio wake katika mkoa wa Ruvuma ni kwa ajili ya mkutano mkubwa wa injili utakaofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Matarawe, Manispaa ya Songea. Aidha, alieleza kuwa ni utamaduni wake kutembelea vituo vya kulelea watoto yatima na wajane kabla ya kuanza mikutano ya injili, kama sehemu ya utumishi wa kiroho.
Kwa upande wake, Mtawa Judith Mwageni, mlezi wa kituo cha St. Anthony, alitoa shukrani kwa ujio huo na msaada uliotolewa, akieleza kuwa kituo hicho kinasimamiwa na Jimbo Kuu la Songea chini ya uongozi wa Askofu Damian Dalu
Miongoni mwa watoto wanaolelewa kituoni hapo, Lea Mbata, alieleza furaha yake kwa kupokea msaada huo na kusema kuwa utawasaidia kwa kipindi kifupi katika mahitaji yao ya kila siku.
Ziara ya Nabii Suguye imetoa faraja kwa watoto yatima na kuonyesha mfano wa upendo wa dhati kwa jamii yenye uhitaji, ikiwa ni sehemu ya maadili ya kiroho na kijamii yanayohamasisha mshikamano na kusaidiana.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa