UTAFITI umebaini kuwa kiasi kikubwa cha sumu kuvu huzalishwa hasa katika mazao ya nafaka kama vile mahindi, karanga na kunde.
Afisa Lishe wa Manispaa ya Songea Anna Nombo anasema sumu kuvu inayojulikana kitaalamu kama mycotoxins, ni aina za kemikali za sumu zinazozalishwa na aina ya ukungu au fangasi wanaoota kwenye mbegu za nafaka kama vile mahindi,karanga, jamii ya kunde, mazao ya mizizi na malisho ya wanyama.
Anasema Sumu kuvu pia hupatikana katika bidhaa za mifugo kama vile maziwa, mayai na nyama pale ambapo chakula kinacholiwa na mifugo kitakuwa kimechafuliwa na sumu hizo.
Anabainisha Zaidi kuwa Baadhi ya sumu kuvu hupatikana kwenye maziwa ya mama anayenyonyesha iwapo atakula chakula kilichochafuliwa na sumu hizo.
Hata hivyo Nombo anasema sumu kuvu haiwezi kuonekana kwa macho, haina harufu, haina kionjo na wala haina rangi. Ukungu unaotokana na sumu kuvu unaweza kuwa na rangi ya kijani, chungwa, kijivu, au njano chafu na unaweza kutoa harufu ya uvundo.
“Binadamu au mnyama anaweza kula sumu kuvu kupitia vyakula vinavyochafuliwa na muda wa kuathiriwa na sumu hiyo unategemea na kiasi cha sumu kuvu kilichomo’’,anasisitiza Nombo.
Tafiti nyingi za kisayansi zimeonesha uhusiano wa sumu kuvu na athari mbalimbali za kiafya kama vile saratani, hasa ya ini, kushusha kinga ya mwili, kudumaa hasa kwa watoto, sumu kwenye figo na vifo kwa binadamu na wanyama ikiwa viwango vya sumu kuvu ni vikubwa.
Baadhi ya sumu kuvu hutoka kwa mama kwenda kwa mtoto akiwa bado tumboni.Hata hivyo athari za kiafya zinaweza kujitokeza baada ya muda mrefu wa matumizi. Sumu inaweza kujirundika na kuendelea kuwa nyingi mwilini kidogo kidogo kulingana na mtu atakavyokuwa anaendelea kula vyakula vilivyo na sumu hiyo.
Kuna njia mbalimbali ambazo mkulima anaweza kuzitumia ili kupunguza uchafuzi wa sumu kuvu katika mazao yake yakiwa shambani au baada ya kuvuna. Njia hizo ni kama zifuatazo
kulima aina za mazao yenye ukinzani dhidi ya kuvu wanaotoa sumu kuvu,kuvuna mazao yakiwa yamekauka vizuri kama inavyoshauriwa na Afisa wa kilimo.
Njia nyingine ni usianike mazao yako kwenye udongo mtupu, Tumia turubai au aina nyingine ya vifaa vya kuanikia au kukaushia mazao,wakati na baada ya kuvuna chambua na kuondoa mbegu zilizooza, zilizovunjika, zilizotobolewa au kuharibiwa na wadudu na zile zilizobadilika rangi.
Hifadhi mazao mahali pakavu na pasipo na joto. Hakikisha mazao yaliyohifadhiwa hayanyeshewi na mvua au kulowa maji.Hifadhi mazao kwenye ghala linaloruhusu mzunguko wa hewa na zuia wadudu waharibifu na kuvu kwa kunyunyiza madawa yaliyokubalika na kushauriwa na wataalamu wa kilimo.
Unaweza pia ukakoboa mahindi na kuchambua vizuri kabla kuyahifadhi ili kuondoa yale yanayoelekea kuwa na uchafuzi wa sumu kuvu ambayo huwa zimeanza kubadili rangi.Kama yanapatikana, tumia dawa Za kibayolojia kama vile Aflasafe.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Mei 28,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa