TAHADHARI YA MAFUTA FEKI YA ALBINO
MFAMASIA Wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Ndavitu Sanga anatahadharisha watu wenye ulemavu wa ngozi(Albino) katika Manispaa hiyo kuwepo kwa mafuta feki ya kupaka aina ya Sunblock cream UV40 kwa ajili ya Albino yanayosaidia kujilinda dhidi ya saratani ya ngozi.
Kulingana na Sanga picha za mkono wa kushoto ndiyo mafuta feki ya albino ambayo yanauzwa kati ya sh.3500 hadi 6000 na picha ya mkono wa kulia ndiyo mafuta halisi ambayo yanauzwa kati ya sh.40,000 hadi 90,000.Sanga ambaye pia ni Mkaguzi wa Vipodozi katika Manispaa ya Songea anasema uchunguzi uliofanywa katika maduka ya vipodozi kwa kushirikiana na uongozi wa Chama cha Albino mkoa wa Ruvuma umebaini mafuta hayo kuuzwa katika maduka ya vipodozi jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
“Hairuhusiwi mafuta ya kupaka Albino aina ya sunblock cream UV40 kuwepo kwenye maduka ya vipodozi badala yake mafuta hayo yanaruhusiwa kuwepo kwenye maduka ya dawa (Pharmacy)’’,anasisitiza Sanga.Hata hivyo Sanga anasema kuanzia mwaka wa fedha wa 2015/2016 Halmashauri ya Manispaa ya Songea imekuwa inatenga bajeti ya sh.milioni 1.5 kwa ajili ya manunuzi ya mafuta ya Albino ambayo wanagawiwa bure katika Kituo cha Afya Mjimwema.
Kwa mujibu wa Sanga bajeti hiyo bado ni ndogo kwa sababu inaweza kununua mafuta kwa Albino 38 tu ukilinganisha na idadi ya Albino 60 waliopo katika Manispaa ya Songea.Amesema katika bajeti ya 2017/2018,Manispaa ya Songea imetenga jumla ya sh.milioni 1.68 kwa ajili ya mafuta hayo ambapo anaitaja changamoto iliyopo ni kwamba mafuta hayo hayapatikani katika katika Hifadhi ya dawa(MSD) badala yake yanauzwa katika maduka ya dawa(pharmacy).
Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 inaonesha kuwa Mkoa wa Ruvuma una jumla ya Albino 523 ambapo Tanzania ina zaidi ya Albino 16,000. Albino wanakabiliwa na changamoto ya ugonjwa wa kansa ya ngozi kutokana na kukosa mafuta hayo hali inayosababisha maisha yao kuwa hatarini.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa