Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Ruvuma imefanikiwa kufuatilia na kuhakikisha kurejeshwa kwa kiasi cha Shilingi Milioni 9.2 za mapato ya ndani zilizokusanywa kupitia mfumo wa kielektroniki na mawakala wa halmashauri lakini hazikuwasilishwa benki kama inavyotakiwa kisheria.
Akizungumza na vyombo vya habari, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma, Bi. Janeth Haule, alisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha nidhamu ya kifedha na uwajibikaji katika taasisi za umma.
Ufuatiliaji huo umechangia kuongezeka kwa makusanyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea, ambapo makusanyo kupitia mfumo wa kielektroniki yamepanda kutoka asilimia 50 hadi asilimia 102 kwenye sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, biashara, ardhi na maliasili.
Aidha, TAKUKURU imetoa ushauri wa kiufundi kuhusu marekebisho ya miradi mitatu yenye thamani ya Shilingi Bilioni 29.9 inayohusisha sekta za miundombinu, kilimo, na fedha, ili kuziba mianya ya rushwa.
Katika kipindi cha Januari hadi Machi 2025, TAKUKURU Ruvuma imefanya chambuzi tatu, warsha tatu, na kufanikisha maazimio 16 ya kuziba mianya ya rushwa. Pia, taasisi hiyo imeendesha semina 24, kuimarisha klabu 53 za kupinga rushwa, mikutano ya hadhara 26, maonesho sita, makala mbili, na vipindi vitatu vya redio.
Programu za uelimishaji zimefanyika katika kata 12, ambako jumla ya kero 118 ziliibuliwa, kati ya hizo, 89 tayari zimetatuliwa na 29 zinaendelea kufanyiwa kazi.
Kwa upande wa malalamiko, TAKUKURU ilipokea jumla ya malalamiko 100, ambapo 80 yalihusu rushwa na 20 hayakuhusu rushwa. Kesi nne zilifikishwa mahakamani na hadi sasa tatu zimeamuliwa kwa ushindi wa Jamhuri.
Bi. Haule ametoa wito kwa wananchi kujiandaa na kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kwa kuepuka vitendo vya rushwa ili kuwachagua viongozi waadilifu watakaolinda maslahi ya umma na kuleta maendeleo endelevu.
Mwisho
AMINA PILLY
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa