TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoani Ruvuma imeokoa zaidi shilingi milioni 43 kutoka Kampuni zinazochimba makaa yam awe katika eneo la Ngaka wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma.
Akitoa taarifa kwa wanahabari katika kipindi cha utendaji kazi cha TAKUKURU mkoani Ruvuma kuanzia Julai hadi Septemba 2019,Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma Yustina Chagaka,amesema fedha hizo zimeweza kulipwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kama ushuru wa huduma.
Chagaka amesema TAKUKURU ilifanya uchunguzi na kubaini kuwa Kampuni hizo zilikuwa hazilipi ushuru wa huduma kwa miaka mingi na kwamba baada ya kubaini hali hiyo ilitoa ushauri kwa mamlaka husika hali hali iliyosababisha Kampuni hizo kuanza kulipa ushuru.
“Fedha hizo zimelipwa ndani ya mwezi Septemba,TAKUKURU katika kipindi hiki imefanya uchambuzi wa mifumo ili kubaini mianya ya rushwa katika ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri za wilaya ya Mbinga,Nyasa,Namtumbo na Tunduru’’,anasema Chagaka.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa TAKUKURU,katika kipindi hicho TAKUKURU ukusanyaji wa kodi kwa kutumia mashine za kielekroniki na kufuatiliaji utoaji wa stakabadhi katika maduka 39 katika Wilaya za Songea,Mbinga,Namtumbo na Tunduru ili kuona iwapo wafanyabiashara wanatoa stakabadhi kwa wateja wao na kama wateja wanaomba stakabadhi baada ya kununua bidhaa.
Hata hivyo amesema katika utafiti huo imebainika kuwa ni asilimia 50 tu ya wenye maduka ndiyo wanatoa risiti na asilimia 50 ya wananchi wanaomba stakabadhi baada ya kununua bidhaa na kusisitiza kuwa elimu inatakiwa kuwa endelevu kwa jamii kuhusu umhimu wa stakadhi baada ya kununua bidhaa.
Chagaka amesema TAKUKURU katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Septemba 2019 ilipokea taarifa 93 kutoka kwa wananchi na amezitaja Taasisi zilizoongoza kwa kulalamikiwa kuwa ni serikali za vijiji na mitaa taarifa 22,Polisi 15,Ardhi 14,Halmashauri saba,Elimu tano na midini taarifa mbili.
Kulingana na Chagaka katika kipindi hicho TAKUKURU imefuatilia miradi ya maendeleo 10 ili kujiridhisha iwapo fedha zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji zimetumika kama ilivyokusudiwa.
Amesema miradi hiyo ipo katika sekta za Ujenzi na Miundombinu,Afya,maji na Barabara yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni tano na kwamba TAKUKURU pia imefuatilia fedha za ruzuku ya elimu zinazotolewa kwa ajili ya uendeshaji wa shule.
”Ufuatiliaji huo umefanyika katika shule za msingi 40 katika kipindi cha Januri hadi Juni 2019,kiasi cha shilingi 98,912,306.02 zimefuatiliwa matumizi yake’’,alisema.
TAKUKURU ni chombo kilichopewa dhamana kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007 ya kuongoza vita dhidi ya rushwa na ufisadi.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Oktoba 16,2019
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa