TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Ruvuma imefanikiwa kuokoa zaidi ya shilingi milioni 21 katika sekta ya afya na elimu ambazo zingeweza kutumika kama mishahara hewa na kuikosesha serikali mapato yake.
Akizungumza na wanahabari ofisini kwake wakati anatoa taarifa ya utendaji kazi wa TAKUKURU katika mkoa wa Ruvuma katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Septemba 2018,Naibu Mkuu wa TAKUKURU katika Mkoa wa Ruvuma Owen Jasson amesema kati ya fedha hizo zaidi ya shilingi milioni 21 zimeokolewa kutoka idara ya afya na shilingi 220,00 kutoka idara ya elimu na kwamba fedha hizo zimerejeshwa serikalini.
Amesema katika kipindi hicho TAKUKURU mkoa wa Ruvuma imepokea taarifa 76 kutoka kwa wananchi kupitia vyanzo mbalimbali na amezitaja Idara zinazoongoza kwa kulalamikiwa kuwa ni Serikali za Mitaa zimepokelewa taarifa 15,Halmashauri taarifa 10,Ardhi 8,Mahakama 8,Elimu 7,sekta binafsi 5,Taasisi za Fedha 4,polisi 4,Afya 2,vyama vya ushirika 2,madini 2,maji moja,mifuko ya hifadhi jamii ma huduma za umeme taarifa moja.
Hata hivyo idadi ya kesi zilizoendelea mahakamani amezitaja kuwa ni 12 na kwamba kati ya kesi hizo sita zilisikilizwa ,kukamilika na kutolewa maamuzi ambapo katika kipindi hicho ni kesi moja mpya ilifunguliwa kutoka katika wilaya ya Namtumbo.
Jasson ameitaja mikakati ya TAKUKURU katika Mkoa wa Ruvuma ni kuhakikisha inapunguza na kumaliza kero kwa wananchi hasa katika maeneo yanayoongoza kwa kulalamikiwa na kwamba TAKUKURU itaendelea kufanya tafiti ndogo katika Idara mbalimbali za Umma zinazolalamikiwa ili kubaini mianya ya rushwa na kupendekeza njia madhubuti za kuziba mianya hiyo kwa manufaa ya wananchi.
"Kuna baadhi ya wananchi bado wanafikiri kuwa mapambano haya ni ya TAKUKURU peke yake,ndiyo maana kuna baadhi ya kesi zimefutwa kwa sababu tu mashahidi walikimbia hawakufika mahakamani kutoa ushahidi hivyo washitakiwa kuachiwa huru'',amesema Jasson.
Ametoa rai kwa wananchi wote mkoani Ruvuma kuendelea kutoa ushirikiano na TAKUKURU katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kutoa taarifa katika ofisi za TAKUKURU zilizopo katika wilaya au kwa viongozi mbalimbali wa serikali.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Novemba 23,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa