Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania ‘TALGWU ‘ Ashiraff Chussi ameendesha zoezi la uchaguzi wa Matawi 6 yenye jumla ya wanachama 558 katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea hapo jana 21 aprili 2021 uliofanyika kwa nyakati tofauti katika ukumbi wa Ushirika Songea Mjini.
Chussi alisema Chama cha TALGWU kinafanya kazi kwa mujibu wa katiba toleo la mwaka 1995 ambacho kiliundwa chini ya sheria ya vyama vya wafanyakazi NA.10 Ya mwaka 1998.
Alisema kuwa kwa mujibu wa katiba ya chama hicho imewataka kufanya uchaguzi wa matawi, Mkoa kila baada ya miaka 5 mitano kwa lengo la kuwapata viongozi wapya ambao watakuwa wanasimamia na kutatua kero zinazowakabili wanachama wa chama hicho.
Chama hicho chenye muundo wa uongozi kuanzia ngazi ya chini ( matawini, Wilaya, Mkoa na Taifa) ambapo kabla ya kuendesha taratibu za uchaguzi huo, Chama hicho hutangaza nafasi mbalimbali za uongozi ambazo hugombewa na wagombea ambao ni watumishi wanachama wa TALGWU ikizingatiwa sheria na kanuni zilizowekwa.
Katika kutekeleza hilo chama cha TALGWU Mkoa wa Ruvuma kimekamilisha kusimamia mwenendo mzima wa uchaguzi katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea ambapo kimefanikiwa kuwapata viongozi wapya wa matawi kwa nafasi mbalimbali za uongozi wa mwenyekiti, katibu na wajumbe wake.
Aliongeza kuwa uchaguzi huo unaendelea kufanyika kwa kila Halmashauri zote 8 nane zilizopo Mkoani Ruvuma na baada ya kukamilika kwa matawi yote kutafanyika uchaguzi ngazi ya Mkoa ambao unatarajia kufanyika kuanzia mwezi julai 2021.
Akibainisha majukumu ya viongozi hao waliochaguliwa kwa mujibu wa katiba ya TALGWU ambayo inawataka kufanya kazi kwa weredi ikiwemo na kutetea haki za wafanyakazi, kuboresha na kuendeleza hali nzuri za wanachama wakiwa kazini, kutoa elimu kwa wanachama kuhusu nidhamu kwa watumishi mahala pa kazi na kuondoa migogoro kati ya mwajiri na mwanachama. “ Chussi alisisitiza”.
Amewataka wanachama wa TALGWU Mkoani Ruvuma kujitokeza kwa wingi wakati zinapotangazwa nafasi mbalimbali za uongozi kupitia Chama cha TALGWU kuanzia ngazi ya Matawi ili kujijengea uwezo na kujiamini na kumwezesha mwanachama kuwa na sifa za kugombea nafasi mbalimbali ngazi ya juu( Mkoa na Taifa ).
Amewatoa hofu wanachama wa TALGWU juu ya upatikanaji wa t-shirt za Mei Mos kuwa ofisi yake tayari imeshapokea t-shirt ambazo zitagawiwa mara baada ya taratibu za kiofisi kukamilika.
Mei Mos mwaka 2021 itafanyika kimkoa Wilayani Nyasa.
IMEANDALIWA NA,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA.
22.04.2021
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa