SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco), limesema linazalisha umeme wa kutosha mahitaji ya nchi, huku ziada ikiwa ni zaidi ya megawati 200 na hivyo kupelekea kupungua kwa changamoto ya kukatika umeme mara kwa mara.
Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk. Tito Mwinuka, wakati akiwasilisha taarifa ya shirika hilo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
Alisema umeme unaozalishwa sasa ni takribani megawati 1517.47, huku matumizi yakiwa ni takribani ni megawati 900.
Dk. Mwinuka alisema shirika hilo linaendelea na juhudi za kuwaunganishia umeme wananchi, kazi ambayo inakwenda sambamba na kuimarisha mifumo ya usafirishaji na usambazaji wa umeme ili kupunguza matukio ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.
Kutokana na jitihada hizo, mapato ya Shirika yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka na kuliwezesha Shirika kujiendesha bila kutegemea ruzuku kutoka serikalini tangu mwaka 2015/16.
“Mapato ya Shirika yameendelea kuimarika, ambapo katika kipindi cha mwaka 2017/18, makusanyo yamekuwa ya wastani wa shilingi bilioni 38 hadi 39 kwa wiki kutoka wastani wa shilingi bilioni 34 katika mwezi Aprili, 2018,” alisema Dk. Mwinuka.
Akizungumzia suala la deni la Tanesco, Dk. Mwinuka, alisema kuna sababu mbalimbali zinazopelekea deni la Shirika kuongezeka, ikiwa ni pamoja na gharama kubwa za uzalishaji wa umeme katika maeneo yaliyopo mbali na gridi ya Taifa ambapo Tanesco hulazimika kuzalisha umeme kwa wastani wa Sh 763 kwa uniti moja.
Alieleza juhudi mbalimbali zinazofanywa na Tanesco ili kupunguza madeni kwa shirika ni kutafuta mikopo yenye masharti nafuu, kuongeza mapato na kupunguza.
CHANZO NI MTANZANIA AGOSTI 29,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa