Uwajibikaji na uadilifu kwa wataalamu ni muhimu katika kusimamia zoezi la uhakiki wa Walengwa wa kaya maskini TASAF ambao utasaidia kupata Takwimu sahihi za wanufaika Halisi ndani ya Manispaa ya Songea.
Kauli hiyo imetolewa na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji TASAF Daniel Makinda katika mafunzo ya wakuu wa Idara na Vitengo yanayohusu Utekelezaji wa kipindi cha pili cha awamu ya tatu TASAF yanayoendelea kufanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea kuanzia 29-30/06/2020.
Makinda alisema, Lengo kuu la mafunzo haya ni kuwajengea uwezo wa kiutendaji katika kusimamia Uhakiki wa kaya maskini utakaofanyika mara baada ya mafunzo hayo ili kupata Takwimu HALISI za Walengwa HALISI ambao wamefariki (ambao walikuwa ni kaya ya mtu mmoja asiye na mtegemezi, kaya ambayo imehama, kaya ya Kiongozi wa Kijiji, kaya ya mjumbe wa Kamati ya Usimamizi ya Jamii (CMC), kaya ambayo haikufika kuchukua malipo yake mara mbili mfululizo. Takwimu hizo zitakusanywa kwa njia ya DODOSO, na kuingizwa kwenye Mfumo wa Takwimu.
Alisema “Manispaa ya Songea ina wanufaika TASAF 4822, kwa mitaa 53 katika kata 21 zilizopo manispaa ya Songea ambazo zinapata huduma ya TASAF. Aliongeza kuwa Utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini pia umewezesha kaya za walengwa kujikita kwenye shughuli za kukuza kipato na kujiimarisha kiuchumi ikiwemo ufugaji, uvuvi, kilimo na biashara ndogo ndogo.
Aliongeza kuwa, zipo baadhi ya kaya za wananchi wanaoishi katika hali duni kwenye maeneo ambayo hayakufikiwa, Hivyo Kipindi cha Pili katika Awamu ya Tatu ya TASAF kaya zote zinazoishi katika mazingira duni zipate usaidizi wa Serikali kupitia TASAF kwa kuwawezesha kufanya kazi na kupambana na umaskini.”
Aliongeza kuwa, Mkazo mkubwa katika Kipindi cha Pili utawekwa katika kuwezesha Kaya zitakazoandikishwa kwenye Mpango kufanya kazi ili kuongeza kipato na kuhakikisha kwamba huduma za jamii zinaongezwa na kuboreshwa na kuendeleza rasilimali watoto hususani katika upatikanaji wa elimu na afya.
Aliwasisitiza Viongozi hao kufanya kazi kwa uadilifu na weredi wakati wa utekelezaji wa Zoezi hili kama maagizo yaliivyotolewa na Mh Rais katika hotuba yake wakati wa uzinduzi wa Kipindi cha Pili kuhusu uwepo wa kaya hewa. “Nanukuu. “ Uwepo wa kaya hewa katika maeneo ya utekelezaji ni aibu sana kwa viongozi wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri. Nitoe wito kwa wahusika wote kusimamia vizuri mradi huu. Serikali haitakuwa na huruma kwa mtu yeyote. Kufanikiwa ama kutofanikiwa kwenye maeneo yenu itakuwa mojawapo ya vipimo nitakavyotumia kujua kama mnastahili kuendelea na nafasi mlizonazo au la. Siwatishi lakini huo ndio ukweli” mwisho wa kunukuu.
Mwisho aliwakumbusha wananchi wote kuchukua tahadhari ya ugonjwa hatari wa COVID-19 ili kuepuka Mikusanyiko isiyoyalazima, kuvaa barakoa, kuepuka kushikana mikono na kunawa mikono kwa sabuni kwa kutumia maji safi yanayotiririka pamoja na kutumia vitakasa mikono.
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY,
KAIMU AFISA HABARI-MANISPAA YA SONGEA.
30.06.2020
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa