Kwa miaka mingi mji wa Songea umekuwa unakabiliwa na mgawo mkali wa umeme hali ambayo imekuwa inarudisha nyuma maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika mji huo ambao ndiyo kioo cha Mkoa wa Ruvuma.
Tangu mwaka 2016 tatizo la mgawo wa umeme katika mji wa Songea limebakia kuwa historia mara baada ya TANESCO Ruvuma kuanza kununua umeme wa maji kutoka Tulila mto Ruvuma.
Chanzo hicho kinamilikiwa na watawa wabenediktine wa Mtakatifu Agnes Chipole Jimbo Kuu Katoliki la Songea ambapo sasa tatizo la umeme katika mji wa Songea limebakia kuwa historia.
Akizungumza kwa niaba ya Mama Mkuu wa Shirika hilo,Sr.Richards Chiwinga(OSB) anasema wana mashine mbili ambazo zina uwezo wa kuzalisha megawatts tano ambapo TANESCO Ruvuma ndiyo wateja wao wakuu ambao wanawauzia umeme huo.
“Mji wa Songea unahitaji megawatts kati ya 3.5 hadi 4.5 hivyo tunabakiwa na ziada ya umeme,TANESCO wamezima majenereta yao chakavu ambayo yalikuwa yanasababisha mgawo wa umeme, hivi sasa wanatumia umeme wetu wa maji unaozalishwa toka hapa’’,anasisitiza Sr.Chiwinga.
Hata hivyo anasema ili kufanikisha mradi huo mkubwa wa umeme Shirika lilipata ufadhili toka kwa raia mmoja wa nchini Uswis anayefahamika kwa jina la Robert Fuchs ambaye alikopa mkopo toka Benki ya Dunia kiasi cha dola za Marekani milioni 30 ambazo zimetumika kujenga mradi huo na kwamba shirika linarudisha mkopo huo kidogo kidogo.
Hata hivyo Sr.Chiwinga anabainisha kuwa ujenzi kamili wa mradi huo ulianza mwaka 2012 na kwamba shughuli za ujenzi huo zilikamilika Septemba 2014 na kwamba tayari kampuni hiyo imekabidhi mradi huo kwa shirika hilo.
Anasema bwawa la Tulila lina ukubwa wa meta za ujazo milioni 1.14,likiwa na urefu wa meta 750 toka usawa wa bahari na usawa wa maji(level) ni meta 748 na kwamba maji yakizidi kiwango hicho yanamwagika.
Mahitaji ya umeme katika mji wa Songea ni kilowatts 4300 hivyo basi kutokana na umeme wa maji unaozalishwa Tulila,TANESCO Ruvuma imefanikiwa kumaliza kabisa tatizo la mgawo wa umeme katika mji wa Songea.
Hata hivyo TANESCO kwa kushirikiana na ufadhili wa serikali ya Sweden,imeaanza utekelezaji wa mradi wa umeme wa Gridi ya Taifa kutoka Makambako hadi Songea ambao unatarajia kuwashwa mjini Songea Septemba 2018.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa habari Manispaa ya Songea
Mei 11,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa