TANGU mwaka 2016 tatizo la mgawo wa umeme katika mji wa Songea limebakia kuwa historia mara baada ya TANESCO Ruvuma kuanza kununua umeme wa maji kutoka Tulila mto Ruvuma.
Chanzo hicho kinamilikiwa na watawa wabenediktine wa Mtakatifu Agnes Chipole Jimbo Kuu Katoliki la Songea ambapo sasa tatizo la umeme katika mji wa Songea limebakia kuwa historia.
Akizungumza kwa niaba ya Mama Mkuu wa Shirika hilo,Sr.Richards Chiwinga(OSB) anasema wana mashine mbili ambazo zina uwezo wa kuzalisha megawatts tano ambapo TANESCO Ruvuma ndiyo wateja wao wakuu ambao wanawauzia umeme huo.
“Mji wa Songea unahitaji megawatts kati ya 3.5 hadi 4.5 hivyo tunabakiwa na ziada ya umeme,TANESCO wamezima majenereta yao chakavu ambayo yalikuwa yanasababisha mgawo wa umeme, hivi sasa wanatumia umeme wetu wa maji unaozalishwa toka hapa’’,anasisitiza Sr.Chiwinga.
Hata hivyo anasema ili kufanikisha mradi huo mkubwa wa umeme Shirika lilipata ufadhili toka kwa raia mmoja wa nchini Uswis anayefahamika kwa jina la Robert Fuchs ambaye alikopa mkopo toka Benki ya Dunia kiasi cha dola za Marekani milioni 30 ambazo zimetumika kujenga mradi huo na kwamba shirika linarudisha mkopo huo kidogo kidogo.
Hata hivyo anazitaja changamoto ambazo zinaukabili mradi huo ni uwepo wa magugu maji kwenye chanzo ambayo yaathiri maji na changamoto kubwa ni Mwekezaji wa kilimo cha umwagiliaji wa zao la kahawa katika kijiji cha Lipokela wilaya ya Songea ambaye anasababisha wakati fulani maji kupungua na kuathiri mradi huo.
Akizungumzia historia ya mradi wa umeme wa Tulila,Sr.Veritas Ndumbili (OSB) ambaye ni mtaalam wa umeme wa maji anabainisha kuwa ujenzi wa bwawa hilo ulianza tangu mwaka 2010 ambapo kampuni ya kutoka nchini China ndiyo ilishinda tenda ya kujenga mradi huo.
Hata hivyo Sr.Ndumbili anabainisha kuwa ujenzi kamili wa mradi huo ulianza mwaka 2012 na kwamba shughuli za ujenzi huo zilikamilika Septemba 2014 na kwamba tayari kampuni hiyo imekabidhi mradi huo kwa shirika hilo.
“Kazi iliyobaki ni yetu sisi,hadi sasa tuna mashine mbili zenye uwezo wa kuzalisha megawati tano,lengo ni kuzalisha umeme megawati 7.5 kwa hiyo tutaongeza mashine moja yenye uwezo wa kuzalisha megawati 2.5’’,anasisitiza Sr.Ndumbili.
Anasema bwawa la Tulila lina ukubwa wa meta za ujazo milioni 1.14,likiwa na urefu wa meta 750 toka usawa wa bahari na usawa wa maji(level) ni meta 748 na kwamba maji yakizidi kiwango hicho yanamwagika.
Kulingana na Sr.Ndumbili, Shirika katika eneo hilo la Tulila, linamiliki eneo lenye ukubwa wa ekari 1000 ambapo wanatarajia pia kuweka maeneo mazuri kwa ajili ya fukwe kupiga picha,kufanya pikiniki na kuogelea lengo likiwa ni kufungua milango ya utalii kwa wageni wa ndani na nje ya nchi katika eneo hilo.
Changamoto kubwa inaoukabili mradi huo wa maji ni magugu maji ambayo yanasababisha mashine kujizima hivyo ili kukabiliana na hali hiyo Shirika limemwajiri kijana ambaye kila siku anaingia kwenye bwawa kuondoa magugumaji hayo.
Hata hivyo Sr.Ndumbili anaitaja changamoto kubwa ambayo inahatarisha uzalishaji wa umeme kuwa endelevu ni uwepo wa Mwekezaji katika shamba la kahawa eneo la Lipokela ambaye anatumia maji ya mto Ruvuma kumwagilia anasababisha upungufu wa maji unaoweza kuathiri uzalishaji wa umeme.
“Kwa kweli Mwekezaji huyo amekuwa anatusababishia tukose maji hapa,tunaomba serikali itusaidia,yeye anatumia maji mengi sana,kwa mfano mwezi Mei mwaka huu maji yalikata ghafla hapa, tulimfuata Mwekezaji,kumbe alikuwa ameingiza maji kwenye mitambo yake tulivyompigia kelele ndipo alifungulia,siku ya pili maji yakaanza kushuka kwetu’’,anasema.
Anasisitiza kuwa ni vema serikali imtafutie Mwekezaji huyo eneo la chini zaidi ili awekeze kwenye kilimo chake kwa sababu kuna siku watashindwa kuzalisha umeme na kuleta matatizo kwa watumiaji wa umeme katika mji wa Songea na vijiji vya wilaya za Songea na Mbinga.
Mahitaji ya umeme katika mji wa Songea ni kilowatts 4300 hivyo basi kutokana na umeme wa maji unaozalishwa Tulila,TANESCO Ruvuma imefanikiwa kumaliza kabisa tatizo la mgawo wa umeme katika mji wa Songea.
Kuanzia Septemba 2018 serikali imeunganisha mkoa wa Ruvuma na Grid ya Taifa katika mradi ambao umeanzia Makambako hadi Ruvuma uliogharimu zaidi ya bilioni 216.
Sera ya Serikali katika umeme ni kuhakikisha wananchi wengi wanapata nishati ya umeme,ingawa takwimu hivi sasa zinaonesha kuwa wananchi wanaopata nishati ya umeme nchini imepanda toka asilimia 10 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 67 mwaka 2017.
Imeandaliwa na Albano midelo
albano.midelo@gmail.com,simu 0784765917.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa