UGONJWA WA AJABU TISHIO KWA WANAFUNZI
UGONJWA wa ajabu ambao umezuka katika shule ya msingi Subira iliyopo katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma tangu Machi mwaka huu bado ni tishio kwa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Majidu Ngonyani amesema tangu kufunguliwa kwa shule hiyo Septemba 18 mwaka huu hadi jana wanafunzi 45 wameathirika na ugonjwa huo hali inayoathiri taaluma katika kiwango cha kutisha.
Amesema jana pekee wanafunzi 27 wameanguka na kupoteza fahamu na kwamba wanafunzi waliokuwa na moyo wa kuhudhuria masomo licha ya kuwepo kwa ugonjwa huo wa ajabu,wameanza kuingiwa na wasiwasi hivyo kuacha kuhudhuria masomo.
Takwimu za mahudhurio ya wanafunzi za leo Septemba 26 zinaonesha kuwa jumla ya wanafunzi 250 wamehudhuria masomo sawa na asilimia 48 kati ya wanafunzi 539 walioandikishwa katika shule hiyo.
Kwa mujibu wa Mwalimu wa Taaluma wa shule hiyo Sarah Haule,wanafunzi wanaopata ugonjwa huo ni wa kike na kwamba hadi sasa licha ya madaktari kuchukua vipimo kwa wanafunzi wanaugua bado haijafahamika ni ugonjwa gani unaowasumbua.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Alhaji Abdul Hassan Mshaweji na Maafisa wa Idara ya Elimu Msingi Manispaa hiyo mara kadhaa wamefanya ziara katika shule hiyo ili kujaribu kutafutia ufumbuzi wa kudumu,hata hivyo hali inazidi kuwa mbaya.
Katika kikao cha Julai 21 mwaka huu,Kamati ya Shule,walimu na wananchi walikubaliana kufanya maombi maalum yaliyoshirikisha madhehebu mbalimbali ya dini ambayo waliaamini yangeweza kumaliza tatizo.
Kuanzia Alhamis iliyopita hadi Kesho Jumatano Septemba 27,waumini wa dhehebu la SILOAM wanafanya maombi ya siku saba mfululizo katika shule hiyo,hata hivyo bado tatizo linaendelea na kuiacha shule hiyo njia panda.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo amesema licha ya kufanyika maombi yalioshirikisha madhehebu yote,bado tatizo la kuanguka kwa wanafunzi linaendelea ambapo ametahadharisha kuwa kuna hatari ya utoro kuongezeka kwa sababu ya kasi ya kuanguka na kupoteza fahamu idadi kubwa ya wanafunzi.
Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Songea leo amefanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Subira katika harakati za kutafutia ufumbuzi wa kudumu tatizo hilo linalowakabili wanafunzi wa kike pekee.
Tatizo lililoikumba shule hiyo limewahi kutokea katika shule ya sekondari Beroya,shule ya msingi Mwengemshindo na Chandarua katika Manispaa ya Songea ambayo ufumbuzi wake ulifanywa kwa maombi maalum ya madhehebu ya dini.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa