JUMLA ya watu 323 wamefariki Dunia katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea kutokana na ugonjwa wa malaria.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Songea Dkt.Mameritha Basike Amesema vifo hivyo ambavyo vilitokea mwaka 2018 ni sawa na asilimia 60.83 ya vifo vyote 531 vilivyotokea kutokana na magonjwa mengine.
Hata hivyo Dkt.Basike amewataja Watoto chini ya miaka mitano waliokufa kutokana na ugonjwa wa malaria ni 65 sawa na asilimia 16.71 ya vifo vyote vilivyotokea kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano ambavyo ni 389.
Takwimu za Idara ya Afya katika Manispaa ya Songea za mwaka 2018 ,zinaonesha kuwa waliougua ugonjwa wa malaria na kupata matibabu ya nje ni 27,202 ambayo ni sawa na asilimia 9.22 ya wagonjwa wote 295,010 waliopata matibabu ya nje.
Kulingana na takwimu hizo,wagonjwa waliougua ugonjwa wa malaria na kulazwa kwa mwaka 2018 ni 3209 sawa na asilimia 11.09 ya wagonjwa wote 28913 waliolazwa.
Dkt,Basike anasema kuwa Watoto chini ya umri wa miaka mitano waliougua ugonjwa wa malaria na kutibiwa kwa matibabu ya nje walikuwa 9561 sawa na asilimia 7.719, ya wagonjwa wote 123,862 chini ya miaka mitano waliopata matibabu ya nje.
Hata hivyo takwimu za mwaka 2017 zinaonesha kuwa waliougua ugonjwa wa malaria walikuwa 48146 sawa na asilimia 3.1 ya wagonjwa 156,479 waliopata matibabu ya nje. Waliougua ugonjwa wa malaria na kulazwa walikuwa 3821 sawa na asilimia 0.14 ya wagonjwa wote 28,136 waliolazwa.
Anavitaja vifo vilivotokea kutokana na ugonjwa wa malaria kwa mwaka 2017 vilikuwa 99 sawa na asilimia 29 ya vifo vyote 341 vilivyotokana na magonjwa mengine na kwamba Watoto chini ya miaka mitano waliokufa kutokana na malaria walikuwa 45 sawa na asilimia 18 ya vifo vyote 244 vilivyotokea kwa magonjwa mengine kwa watoto chini ya miaka mitano.
Katika kupambana na Malaria,Dkt.Basike anasema Halmashauri ya Manispaa ya Songea imekuwa ikikabiliana na changamoto mbalimbali zikiwemo,Baadhi ya jamii katika Manispaa ya Songea kutozingatia maelekezo ya matumizi sahihi ya vyandarua na matibabu sahihi,akinamama kutowahi kliniki mara anapojihisi kuwa mjamzito na hivyo kuchelewa kupata Tiba za tahadhari.
Hata hivyo Afisa Afya wa Manispaa ya Songea Vitalis Mkomela amesema Halmashauri hiyo ina mpango wa kuua viluilui vya mbu kwenye mazalia ambapo Kwa mwaka 2018 Halmashauri ya Manispaa ya Songea imeuwa viluilui vya mbu kwa kupulizia kwenye mazalia ya wazi (madimbwi, mabwawa ya samaki,) mita za mraba 32,000 na mazalia yaliyofunikwa (kwenye makalo )mita za ujazo 50,000 na kwamba Mpango huu ni endelevu.
Naye Mganga Mfawidhi Kituo cha Afya Mjimwema Grace Daniel Ndumbaro akizungumza ofisini kwake amesema kuwa ugonjwa wa malaria umepungua kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na wakati wa nyuma ambapo wamepiga vita kwa asilimia 80 hadi 90 katika Manispaa ya Songea.
Ndumbaro ameishukuru Serikali na vyombo vya habari kwa kusaidia kutoa elimu kuhusu ugonjwa wa Malaria na utoaji wa vyandarua kwa wajawazito na watoto chini ya miaka mitano, pia ameiomba Serikali kuboresha na kuongeza miundo mbinu mbalimbali kama vile dawa, gari ya kubebea wagonjwa (Ambulance) na X-Ray.
Seleman Yusuph ni Mganga katika Kituo cha Afya Mjimwema ameeleza kuwa wagonjwa wa Malaria wamepungua hadi watu 100 kwa msimu huu wa kiangazi na ameshauri watu watembelee vituo vya afya na kuachana na tiba za mitaani pale wanapohisi dalili za malaria.
Imeandaliwa na
Jamila Ismail
Wa kitengo cha TEHAMA Manispaa ya Songea
Agosti 7,2019.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa