SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) linatarajia kuanza kununua mahindi toka katika Mkoa wa Ruvuma ambao ni miongoni mwa mikoa ambayo ni magwiji wa uzalishaji wa mazao ya chakula.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema ujio wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la WFP David Beasley hapa nchini ni fursa itakayowawezesha Watanzania kunufaika kwa kiwango kikubwa katika kilimo, uhifadhi na uuzaji wa mazao ya chakula yanayolimwa hapa nchini.
Waziri Mkuu amesema Tanzania inatarajiwa kuwa na ziada ya chakula msimu wa mavuno utakapokamilika mwaka huu hivyo itahitaji kupata soko nje ya nchi ili iweze kuuza ziada hiyo.
“Taarifa za Wizara ya Kilimo zinaonesha kuwa mavuno ya mazao ya chakula kama mahindi, maharage na mbaazi yatafikia tani milioni 16 wakati mahitaji ya chakula kwa Watanzania kwa mwaka ni tani milioni 13, hivyo tutakuwa na ziada ya tani milioni tatu,” amesema.
Hatua ya WFP kukubali kununua chakula cha ziada kitakachozalishwa hapa nchini imewahakikishia Watanzania kuwa mazao yao hayatakosa soko.
Mkurugenzi huyo wa WFP ametembelea vijiji kadhaa katika Halmashauri za Songea, Namtumbo na Madaba mkoani Ruvuma amejionea jinsi wananchi walivyopata mavuno mazuri hasa mahindi.
Mkoa wa Ruvuma katika kipindi cha mwaka 2017/2018 umezalisha mahindi tani 933,284.Akitoa taarifa ya NFRA kwa niaba ya Meneja wa Kanda ya Songea Eva Kwavava amesema Mapendekezo ya malengo ya ununuzi kwa mwaka 2018/2019 katika mkoa wa Ruvuma yanaonesha kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Songea mgawo ni tani 417 wakati kiasi kilichozalishwa ni tani 58,144,Halmashauri ya Wilaya ya Songea tani 1,983.531,kiasi kilichozalishwa ni tani 227,320 na Halmashauri ya Madaba tani 1,216.466 na kiasi cha tani zilizozalishwa ni 148,408.
Kulingana na mapendekezo hayo Halmashauri ya wilaya ya Mbinga imepangiwa kununua tani 1,189.175,kiasi kilichozalishwa ni tani 165,484,Halmashauri ya Mbinga Mji tani 461.976 na kiasi cha tani zilizozalishwa ni 64,288.
Katika Wilaya ya Namtumbo zitanunuliwa tani 1,068.017,kiasi kilichozalishwa ni tani 134,708,Nyasa tani 663.011 na kiasi kilichozalishwa ni tani 64,432 na wilaya ya Tunduru imezalisha tani 70,500 za mahindi na hakuna wa ununuzi.
Katika msimu wa mwaka 2017/2018 Kanda ya Songea ilipangiwa kununua mahindi tani 6,182,hata hivyo kanda hiyo ilinunua jumla ya tani 11,557,529 baada ya malengo kuongezwa mara mbili.
Kaimu Meneja wa NFRA Kanda ya Songea amesema katika kituo hicho kilichopo Ruhuwiko mjini Songea,kuna tani 21,892.924 za mahindi ambayo yanatokana na ununuzi wa misimu miwili ya 2016/2017 na 2017/2018 na kwamba akiba hiyo ipo katika hali nzuri.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Julai 30,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa