Kilimo cha miti kimepata umaarufu wa ghafla miaka ya hivi karibuni kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ongezeko la mahitaji ya mazao ya miti.
Wananchi wa mikoa ya kusini ukiwemo mkoa wa Iringa,Njombe na Ruvuma wana fursa kubwa ya kutajirika na miti ya mbao hasa kutokana na hali ya hewa katika mikoa hiyo kuruhusu kustawi vema miti ya mbao ya aina mbalimbali.
Matumizi ya mbao katika kipindi hiki yameongezeka katika kiwango kikubwa kwa sababu miti inatumika kwa mbao, nguzo za umeme, nguzo za kujengea na utengenezeji wa vitu vya thamani .
Hata hivyo Mtaalam wa Shamba la serikali la Misitu Njombe Godwin Mgunda anasema licha ya kuibuka kwa fursa hii,bado wananchi wengi hawajachangamkia fursa ya upandaji miti ambayo inaweza kubadilisha maisha yao baada ya miaka michache.
“Miti inapofikisha umri wa kuanzia miaka saba huwa tayari kwa kuanza kuvunwa kwa mbao ndogo,hekari moja ya shamba inachukua wastani wa miti 600,wastani wa chini wa mti mmoja kwa sasa uliokomaa ni shilingi 30,000 , inategemea na ukubwa wa mti’’,anasisitiza Mgunda.
Anabainisha kuwa iwapo hekari moja ikiwa na miti iliyokomaa inaweza kuingiza mapato ya shilingi milioni 18 na kwamba anasisitiza kuwa Kilimo cha miti ni rahisi kwa sababu ukishapanda hakihitaji uangalizi mkubwa na wala hauhitajiki uwe karibu na shamba muda wote.
“Mvua inyeshe ama isinyeshe mti wa mbao, ukishachipua huwa haufi kwani huendelea kutumia unyevu wa ardhini. Kazi namba moja unapokuwa umeshakamilisha upandaji wa miti kwenye shamba ni kutengeneza njia za kuzuia moto walau mara moja kwa mwaka, kazi ya pili ni kufyekea miti inapokua walau kwa mwaka mara moja’’,anasema Migunda.
Hata hivyo anasema ardhi ni rasilimali inayopanda thamani kila hivyo ukiwa na shamba la miti,thamani ya ardhi hiyo inazidi kupanda kila siku na miti uliyopanda inazidi kupanda thamani kila siku.
Migunda anazitaja huduma ambazo zinatolewa Shamba la Misitu Njombe(Njombe Forest Plantation) kuwa ni kutoa huduma ya upatikanaji wa mashamba ya kupanda miti ya mbao kwa bei ya kati ya shilingi 200,000 hadi 180,000.
Huduma nyingine anazitaja kuwa huduma ya kuzalisha ya miche ya miti ya mbao aina ya mikaratusi na pine na kupanda mashambani bei ya shilingi 100 kwa mche,kutoa huduma ya kusimamia shamba kwa mteja aliye mbali na shamba lake na mteja kuunganishwa na serikali kwa ajili ya taratibu za hati.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Serikalini
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa