SERIKALI kupitia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imeamua kuanzisha kitengo mahususi cha kuvutia utalii wa mikutano kinachojulikana kama 'The National Convention Bureau'.
Kitengo hicho kitakuwa na mamlaka ya kuandaa, kualika na kuvutia mikutano ya kimataifa kufanyika Tanzania.
Mwenyekiti wa TTB, Jaji mstaafu Thomas Mihayo aliwaambia waandishi wa habari mwishoni mwa wiki kuwa chombo hicho kitaanza kama kitengo ndani ya TTB kwa kushirikiana na Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (NICC) ili kufanikisha malengo ya kuvutia utalii wa mikutano na matukio.
"Sekta ya mikutano na matukio (MICE) huzalisha takribani dola za Marekani milioni 300 kwa mwaka, hivyo ni fursa kwa Tanzania kuchangamkia kwani vigezo vyote vya kufanya utalii wa mikutano tunavyo hapa Tanzania," amesema Jaji Mihayo.
Amesema, ushirikiano huu unalenga kuhakikisha shughuli zinazohusu mikutano na matukio zinafanyika kwa utaratibu na utaalamu wa hali ya juu ili kufanikisha soko la utalii wa mikutano na matukio.
Alisema kigezo kikubwa ni kumbi za mikutano, hoteli na usalama ambavyo vyote vinapatikana nchini pamoja na vivutio vya utalii kama mbuga za wanyama na Mlima Kilimanjaro vitakuwa ni sehemu ya kuchochea utalii wa mikutano.
"Mkutano mmoja wa kimataifa huleta watu si chini ya 2000 ambao watahitaji kula, kulala, kufanya matembezi baada ya mkutano hivyo watachochea mzunguko wa fedha na pia watahamasika kutembelea vivutio vya utalii na kupeleka idadi watalii kuongezeka," amesema.
Aliongeza nchi ambazo utalii ni sehemu muhimu ya uchumi kama vile Australia na Malaysia wameanzisha kitengo hicho na kwa Bara la Afrika, nchi ya Rwanda na Afrika Kusini zimeanzisha kitengo hicho na kimewaletea mafanikio kwa kupokea mikutano ya kimataifa nchini mwao.
"Juhudi za makusudi zimechukuliwa na serikali kupitia TTB na AICC kwa kufanya vikao na wadau juu ya uanzishwaji wa kitengo hicho," amesema Jaji Mihayo.
Amesema Bodi ya Utalii imeandaa mafunzo yatakayofanyika mwezi Oktoba kwa wadau kwa lengo la kuhamasisha utalii wa mikutano (MICE) na fursa zinazopatikana kupitia mikutano hiyo.
Wataalamu kutoka nchi za Afrika kusini na Rwanda wanategemewa kuwasilisha mada katika semina hiyo.
Bodi ya Utalii imeendelea kuwa miongoni mwa sekta zinazochangia maendeleo ya uchumi wa Taifa kwa kuchangia asilimia 17.2 ya pato la Taifa zaidi ya asilimia 24 ya mauzo yote ya nje na zaidi ya asilimia 11 ya ajira zote zinazotengenezwa nchini.
CHANZO NI GAZETI LA SERIKALI
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa