MKOA wa Ruvuma una vivutio vingi tofauti ambavyo bado havitumiki katika kuchangia pato la Taifa na kuinua uchumi wa wananchi wa eneo husika.
Jiwe la Mbuji ambalo lipo katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma ni miongoni mwa vivutio adimu na vya kipekee vilivyopo katika Bonde la ziwa Nyasa ambalo linajumuisha mikoa ya Mbeya,Ruvuma na Njombe.
Afisa Maliasili na Utalii wa Mkoa wa Ruvuma Africanus Challe anasema tayari Idara yake imeliingiza jiwe la Mbuji kwenye orodha ya vivutio vya utalii katika Mkoa wa Ruvuma ili hatimaye kazi ya kutangaza eneo hilo na vivutio vingine iweze kufanyika kwa tija.
Kivutio cha jiwe la Mbuji kimekuwa gumzo kwa wengi waliosikia taarifa za kivutio hicho.Neno Mbuji kwa lugha ya kabila la wamatengo ni "Kitu kikubwa",jiwe hili lipo katika kijiji cha Mbuji kata ya Mbujii na limekuwa kivutio adimu kwa wageni wa ndani na nje ya nchi.
Jiwe la Mbuji lina maajabu mengi yakiwemo jiwe pekee kubwa Mkoani Ruvuma,Lina vyanzo vingi vya maji chini yake,ni vigumu kulipanda bila kuwaona wazee kwa sababu ni vigumu kupanda na kulizunguka jiwe hilo bila kufuata mila na desturi za kabila la wazee wa kimatengo.
Unapofika katika jiwe hilo inakulazimu kuwatafuta wazee wanaotoa maelekezo kwa yeyote anayetaka kupanda jiwe hilo,ambalo linaheshimika sana na wakazi wanaolizunguka jiwe hilo.
Utafiti umebaini kuwa,sehemu kubwa ya wananchi wanaolizunguka jiwe jiwe la Mbuji hawajawahi kulipanda wala kulisogelea kwa hofu ya kupoteza maisha.
Mzee Sixmund Ndunguru (90) anasema kuwa ili kupanda jiwe hilo ni lazima uwe na Mwongozaji ambaye ni mzee wa mila ambaye anazifahamu vizuri mila na taratibu za kabila la wamatengo zitakazokuwezesha kupanda jiwe hilo bila matatizo na kufurahia vivutio vilivyopo.
“Ninayafahamu maajabu ya jiwe la Mbuji tangu nikiwa na umri wa miaka mitano,mandhari ya jiwe hili hayajabadilika wala kuharibiwa tangu nilipolifahamu jiwe hili’’,anasema Ndunguru.
Kulingana na Ndunguru,mimea aina ya matete ambayo imekuwepo katika jiwe hilo tangu miaka ya 1940 alipopanda juu ya jiwe hilo kwa mara ya kwanza akiwa na baba yake mzazi na kwamba kila mtu anaruhusiwa kupanda jiwe hilo kwa kuzingatia maelekezo ya wazee wa mila na desturi.
Serikali ya Kijiji cha Mbuji kwa kushirikina na wazee wa mila wameamua kuboresha mazingira ya eneo la kivutio hicho cha utalii kwa kujenga nyumba za mila za wamatengo,kupika vyakula vya asili na ngoma za jadi ili watalii wakishaona jiwe hilo waweze kupata vyakula na ngoma za asili ya wamatengo hivyo wananchi kujipatia kipato.
Makala hii imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa