Afisa Biashara Mkoa wa Ruvuma Joseph Kabalo amesema ili bidhaa ziweze kukamilika katika matumizi yake kwanza zinahitaji zizalishwe kwa ubora, pia ili uzalishaji ufanikiwe nilazima bidhaa ziwafikie watumiaji wa mwisho ( final consumer).
Kauli hiyo imetolewa katika kikao cha wafanyabiashara wazalishaji wa bidhaa za Vipodozi, chaki, na vifaa vya ujenzi “Gypsum powder”, pamoja na wadau mbalimbali wakiwemo na SIDO, TCCIA, TBS na wafanyabiashara wauzaji wa bidhaa hizo, kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea leo 25.09.2020.
Kabalo alisema lengo la kikao hicho ni kufanya utambulisho wa bidhaa ambazo zinazalishwa Manispaa ya Songea, Mkoani Ruvuma ili kuwaunganisha wafanyabiashara wazalishaji wa bidhhaa za vipodozi, chaki, na vifaa vya ujenzi ambavyo vinazalishwa kwa kutumia malighafi ambazo zinazopatiakana ndani ya Mkoa wa Ruvuma.
Aliongeza kuwa viwanda vinavyoanzishwa na wajasiliamali wenyewe endapo bidhaa zake hazitaweza kutumika ipasavyo vitashindwa kujiendesha kwasababu sisi wenyewe hatutaki kuvitumia, alisema endapo bidhaa hiyo itakuwa haijamfikia mtumiaji wa mwisho,pia matumizi ya bidhaa hizo yatakuwa hayajakamilika na mfikishaji wa bidhaa hizi kwa watumiaji wa mwisho ni wafanyabiashara waliopo ndani ya Mkoa wa Ruvuma.
Naye Mkurugenzi wa kampuni Power Body Butter George Ndimbo alisema Kampuni hiyo inazalisha bidhaa za vipodozi vya asili kama vile sabuni ya kuogea, vitakasa mikono, sabuni ya kudekia, sabuni ya kuondoa harufu chooni, mafuta ya kupaka pamoja na rosheni ambazo zina tengenezwa kwa kutumia malighafi zinazolimwa ndani ya Mkoa wa Ruvuma ikiwemo na zao la Mawese ambalo hulimwa Wilaya ya Nyasa.
Ndimbo aliongeza kuwa falsafa ya Tanzania ya viwanda imemsaidia sana kwa kuanzisha kiwanda cha Power Body Butter ambacho licha ya kutengeneza bidhaa hizo, wanakazi nyingine ya kutoa elimu ya afya ya ngozi ili mteja anapotumia bidhaa hizo ngozi yake iwe na muonekano wa kuvutia.
Alibainisha kuwa Power Body Butter yenye makao makuu Mjini Songea kata ya Msamala inazalisha vipodozi vya asili ambavyo vimetengenezwa kwa kiwango chenye ubora na vimethibitishwa na TBS.
Naye Afisa uendeshaji biashara SIDO Ruvuma Linus Kimoro alisema shirika la SIDO linatoa huduma kwa jamii ikiwemo wajasiliamali kwa kuwapatia elimu ya ujasiliamali, kutoa mikopo kwa wajasiliamali, pamoja na kutoa maonesho mbalimbali kwa wajasiliamali.
Naye Afisa biashara Manispaa ya Songea Furaha Mwangakala alisema baada ya kikao hiki cha wafanyabiashara anategemea kuziona bidhaa hizi za vipodozi, chaki na bidhaa za ujenzi zinauzwa kwenye maduka yetu ndani ya Mkoa wa Ruvuma ili uzalishaji uweze kuboreka Zaidi.
IMETAYARISHWA NA;
AMINA PILLY;
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA.
24.09.2020.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa