MANISPAA ya Songea mkoani Ruvuma imeendesha mafunzo ya siku mbili kwa wawezeshaji rika ngazi ya Kata ambapo jumla ya washiriki 42 wamepata mafunzo hayo.
Akisoma taarifa fupi ya mafunzo hayo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mkuu wa Wilaya ya Songea,mmoja wa wawezeshaji rika Mkoa wa Ruvuma Nickson Homange amesema mafunzo hayo yanatolewa kwa siku mbili kila Halmashauri kwa kufuata mwongozo wa kitaifa wa stadiza maisha.
Hata hivyo amessisitiza kuwa mafunzo hayo yatakuwa yanaendeshwa kwa kutegemea mapato ya ndani ya kila Halmashauri au wilaya na kwamba serikali imeamua kuandaa mafunzo hayo kutokana na changamoto zinazowakumba vijana wengi nchini.
“Vijana wengi wamekata tamaa,lakini hawana stadi za maisha za kukabiliana na changamoto hivyo wanaathirika na mambo mengi ya maisha,kiuchumi,kielimu na magonjwa ya kujamiiana na tabia za kujamiana,matumizi ya dawa za kulevya na matatizo ya uzazi,VVU na UKIMWI’’,anasema Homange.
Mwezeshaji huyo amebainisha Zaidi kuwa,Kutokana na changamoto hizo Wizara imeamua kutoa muongozo ili kuwaandaa wawezeshaji rika wawili kila kata ambao watakuwa na miongozo midogo ya kufanya mafunzo katika jamii.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yatawawezesha vijana kuwa wabunifu kwa kuyatumia mazingira yao kubuni kazi za kufanya ili kujipatia kipato na kuwawezesha vijana kuunda vikundi vya uzalishajimali ili asilimia tano ya mapato ya ndani katika Halmashauri yaweze kuwanufaisha vijana wote.
Mgeni rasmi katika Mafunzo hayo alikuwa ni Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Songea mjini Musa Mwakaja ambaye aliwaasa vijana kuwa wasikivu katika mafunzo hayo ili kwenda kutoa habari sahihi kwa vijana wengine ambao watakwenda kuwafundisha katika ngazi ya kata.
Mada zilizofundishwa katika mafunzo hayo ni mzunguko wa maisha ya binadamu,kupevuka na balehe,kuhimili mihemko,mfumo wa uzazi wa binadamu,ngono salama, mawasiliano,mahusiano mema,dawa za kulevya,shughuli za kujipatia kipato,kuepuka mimba za utotoni na uzazi wa mpango.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Mei 17,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa