Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ameongoza wananchi na viongozi mbalimbali Mkoani Ruvuma katika zoezi la uzinduzi wa chanjo ya UVIKO 19 hapo jana tarehe 04 Agosti 2021, tukio ambalo limefanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea, na kuhudhuliwa na viongozi mbalimbali ikiwemo na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri,Wenyeviti wa Halmashauri, Viongozi wa dini pamoja na wananchi.
Akizungumza katika uzinduzi wa chanjo hiyo Ibuge amewataka wananchi Mkoani Ruvuma kuendelea kuchukua tahadhari kwa kufuata muongozo uliotolewa na Wizara ya afya ikiwemo na uvaaji wa barakoa, kutumia vitakasa mikono, kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka, kuepuka mikusanyiko isiyokuwa ya lazima pamoja kukaa umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu pale inapotokea kuna mkusanyiko “Alibainisha”.
Ibuge amewataka viongozi wa Taasisi zote Mkoani Ruvuma kuhakikisha wanasimamia upatikanaji vifaa kinga kwa ajili ya watenda kazi wake kama vile ndoo za maji tiririka na sabuni, barakoa, vipima joto pamoja na vitakasa mikono, vilevile kuwepo na utaratibu wa kupunguza misongamano sehemu za kazi pasipo kuathiri utendaji kazi wa kila siku na shughuli za taasisi husika.
Pia amemtaka kamanda wa jeshi la polisi Ruvuma kuhakikisha wasafiri hawasimamishwi katika vyombo vya usafiri kama vile mabasi na daladala bali wabebe watu sawasawa na idadi ya siti zilizopo kwenye vyombo hivyo sambamba na bodaboda kubeba watu wasiozidi wawili (mishikaki) kwa mujibu wa muongozo wa Wizara ya Afya uliotolewa mwezi Mei 2021 pamoja na vyombo vyote vya mawasiliano Mkoani Ruvuma wakishirikiana viongozi wa dini kutoa elimu kwa jamii juu ya namna ya kujikinga na ugonjwa wa UVIKO 19. ‘Alisisitiza’.
Amewataka viongozi wa Halmashauri zote kusimamia upatikanaji na utumiaji wa ndoo za maji tiririka na sabuni kwenye maeneo yote yanayojumuisha mikusanyiko ya watu kama vile masoko pamoja na stendi zote, pia vituo vyote vya kutolea huduma za afya kuhakikisha wanapunguza msongamano wa watu wanaoenda kuona wagonjwa ili kupunguza changamoto ya ongezeko la watu wenye maambukizi ya UVIKO 19.
Ibuge amewasisitiza viongozi wa dini kufuata muongozo wa namna ya kujikinga na ugonjwa wa UVIKO 19 kwenye maeneo yote ya nyumba za ibada pamoja na kupunguza muda kufanya ibada angalau kwa saa moja, huku akiwataka wakuu wa Idara ya uamiaji kuhakikisha wanawachunguza wahamiaji wote wanaoingia Mkoani Ruvuma ili kujiridhisha kama hawana maambukizi ya UVIKO 19 na hii itasaidia kupunguza maambukiza katika maeneo husika.
Katika kuendelea kuchukua tahadhari ya kujikinga ugonjwa huo Ibuge amezuia kwa muda Mikusanyiko yote isiyokuwa ya lazima kama vile mikutano mikubwa na matamasha mbalimbali ndani ya Mkoa wa Ruvuma na amesisitiza kuwa yeyote atakayekiuka agizo hilo atakuwa amevunja sheria na hatua kali zitachukuliwa dhidi yake, ‘Alieleza’.
Kwa upande wake Mganga mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Jerry Kanga ametoa rai kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupata chanjo ya UVIKO 19 kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa hiyari ili kujikinga na mashambulizi ya virusi vya ugonjwa huo ambapo kwa Mkoa wa Ruvuma umepata jumla ya chanjo elfu thelathini (30000) na kwa Manispaa ya Songea chanjo hiyo inatolewa katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa Songea, Kituo cha afya Mjimwema pamoja na Kituo cha afya Mshangano.
Miongoni mwa viongozi waliopata chanjo ya UVIKO 19 ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea, viongozi wa dini, wataalamu wa afya na wananchi mbalimbali.
IMEANDALIWA NA,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
05.08.2021.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa