MANISPAA ya Songea iliyopo mkoani Ruvuma ni miongoni mwa Halmashauri nchini ambazo zimeweka dhamira ya kuhakikisha inaweka mikakati ya kuboresha maisha ili kuendana na kasi ya Rais wa awamu ya tano ya kujenga Tanzania mpya yenye neema.
Baraza la Madiwani la Manispaa hiyo likiongozwa na Mwenyekiti wake Mstahiki Meya Alhaj Abdul Hassani Mshaweji kwa kushirikiana Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Tina Sekambo pamoja na wataalam katika idara zote wameweka maeneo kumi ya vipaumbele yatakayoiwezesha manispaa hiyo kupaa.
Halmashauri ya Manispaa imeangalia maeneo ya msingi katika kuboresha na kuimarisha utoaji wa huduma kwa kuyapa uzito maeneo hayo ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa majukumu ya msingi ya Halmashauri.
Vipaumbele ambavyo vimepitishwa na Baraza la madiwani la Halmashauri ya manispaa hiyo vimelenga katika Sekta ya Elimu ambapo Halmashauri imejiwekea malengo katika kuboresha huduma za jamii hasa katika kuboresha miundombinu ya shule za Msingi na Sekondari kwa kukamilisha miradi viporo na kujenga miundombinu mipya.
Baraza limeyataja Maeneo yatakayozingatiwa katika sekta ya elimu kuwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa,maabara,mabweni,vyoo, ukarabati wa madarasa ununuzi wa samani pamoja na mishahara ya watumishi.
Sekta ya Afya ni miongoni mwa vipaumbele vilivyopitishwa na Baraza hilo Lengo likiwa ni kuboresha miundombinu ya Vituo vya Afya na Zahanati kwa kuendeleza ujenzi na upatikanaji wa dawa. Maeneo muhimu ni ujenzi wa zahanati, ukarabati, ujenzi wa chumba cha upasuaji, samani na ununuzi wa madawa.
Kipaumbele kingine ambacho kimewekwa na Manispaa ya Songea kuwa ni Sekta ya Maji Lengo likiwa ni kuongeza upatikanaji wa maji ya kutosha katika maeneo ya pembezoni ya Manispaa kwa kujenga visima vya maji virefu na vifupi, kuanzisha uvunaji wa maji ya mvua na kuanzisha mtandao wa maji ya bomba.
Sekta ya ujenzi pia imepewa kipaumbele ambapo Manispaa ya Songea imejiwekea lengo la kuboresha miundombinu ya barabara kwa kufanya matengenezo ya mara kwa mara, maeneo korofi na matengenezo ya kawaida.
Kipaumbele pia kimewekwa katika Sekta ya Kilimo,Uvuvi Mifugo na Ushirika Lengo likiwa ni kuendeleza kilimo bora na endelevu kwa kutumia pembejeo za kisasa kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Sekta ya Mipango Miji, Ardhi na Maliasili ni miongoni mwa vipaumbele vilivyopitishwa katika bajeti lengo likiwa ni kuboresha makazi ya wananchi kwa kuongeza upimaji wa viwanja, na ulipaji wa fidia kuboresha maeneo yaliyoendelezwa kiholela ambayo yamesababishwa na uhaba wa viwanja vilivyopimwa.
Masuala Mtambuka ambayo yamepewa kipaumbele katika manispaa ya Songea ni pamoja na kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi ya maradhi mbalimbali kama UKIMWI, Malaria Kifua Kikuu na kushughulikia masuala ya UKIMWI, magonjwa ambayo hayapewi kipaumbele,Mazingira na kupambana na Madawa kulevya na rushwa.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Mei 14,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa