Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
16 MEI 2022
Waandishi wa habari Ruvuma watakiwa kutumia taaluma zao kuibua vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa lengo la kuzuia na kutokomeza matukio hayo katika jamii.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa maadili ya kamati ya waandishi wa habari Mkoa wa Ruvuma Methew Ngalimanayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari pamoja na wadau wa habari kwenye maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani ambapo kwa Mkoa wa Ruvuma yameadhimishwa leo tarehe 16 Mei 2022 katika ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Ngalimanayo pia ametoa rai kwa waandishi wa habari kuhakikisha usalama wao wakati wakitekeleza majukumu yao na kufuata maadili ya uandishi wa habari pamoja na kutumia mbinu za kujilinda na matukio yenye kuathiri taaluma yake.
Ametoa wito kwa waandishi hao kutumia nafasi yao katika jamii kwa kuvitangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo ndani ya Mkoa wa Ruvuma ili kuutambulisha Mkoa ndani na nje ya nchi pamoja na kuvutia wawekezaji na kusaidia kukuza uchumi wa Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Ruvuma Amoni Mtega alisema kuwa lengo la kuadhimisha siku hiyo ni kulinda hali ya uwepo wa uhuru wa vyombo vya habari na kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili waandhishi wa habari katika kutimiza majukumu yao pamoja na kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo.
Naye Katibu wa Klabu ya waandishi wa habari Mkoani Ruvuma Andrew Chatwanga alisema kuwa maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari Tanzania yalianza kuadhimishwa rasmi mnamo mwaka 1993 baada ya kuratibiwa na Umoja wa Mataifa kwa lengo la kutambua mchango wa sekta ya habari na kuangalia changamoto zinazoikumba sekta hiyo.
Akiwasilisha mada katika mkutano huo Mhdhili Dkt. Denis Mpagaze alisema kuwa miongoni mwa changamoto kubwa katika tasnia ya habari ni ukuaji wa teknolojia hali inayopelekea watu wasio waandishi wa habari kufanya kazi za habari kwa kutumia mitandao ya kijamii na kutoa taarifa ambazo siyo sahihi na zisizozingatia maadili ya uandishi wa habari.
Aliongeza kuwa ili kukabiliana na changamoto hizo Serikali iangalie namna ya kudhibiti hali hiyo kwa kuweka sheria kali zaidi pamoja na waandishi wa habari kwenda sambasamba na ukuaji wa teknolojia katika nyanja ya habari bila kuhatarisha maisha yao.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Dkt. Frederick Sagamiko alisema kuwa Halmashautri ya Manispaa ya Songea itaendelea kushirikiana na waandishi wa habari Mkoani Ruvuma kwa lengo la kutoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo kwa wananchi.
Dkt. Sagamiko ametoa rai kwa waandishi wa habari kushiriki katika kuleta maendeleo Mkoani Ruvuma kwa kutangaza fursa mbalimbali za maendeleo zinazopatikana ndani ya Mkoa kama vile uwekezaji wa viwanda na utalii.
Maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani hufanyika kila mwaka Mwezi Mei na kwa Mkoa wa Ruvuma yamefanyika leo na kuwashirikisha wanahabari na wadau mbalimbali wa habari wakiwemo viongozi wa Serikali ambapo maudhui ya maadhimisho hayo kwa mwaka 2022 yanasema “Uandishi wa habari na changamoto ya kidigitali”.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa