WAGONJWA 24 WAFANYIWA UPASUAJI KITUO CHA AFYA MJIMWEMA
MGANGA Mkuu wa Manispaa ya Songea Dk.Mameritha Basike amesema kitengo cha upasuaji katika kituo cha Afya Mjimwema kimefanikiwa kuwafanyia upasuaji wagonjwa 24 ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.
Amesema wagonjwa wote waliofanyiwa upasuaji wanaendelea vizuri na kwamba wananchi wa Manispaa ya Songea hivi sasa wamehamasika kukitumia kituo hicho ambacho kilianza rasmi kutoa huduma za upasuaji Agosti 8 mwaka huu.
Hata hivyo amesema kitengo hcho kinakabiliwa na upungufu wa vifaa ambapo serikali katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2017/2018 imetenga kiasi cha sh.milioni 40 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya upasuaji katika kituo hicho.
Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dk.Hamisi Kigwangalla akiwa mjini Songea amewahakikishia wananchi wa Manispaa ya Songea kuwa Kituo cha Afya Mjimwema kilichopo katika Manispaa hiyo kitapandishwa hadhi kuwa hospitali ya Wilaya.
Dk.Kigwangalla alitoa ahadi hiyo kabla ya kuzindua mradi wa uchunguzi wa saratani za mlango wa kizazi,matiti na magonjwa yasiyoambukiza katika uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Kituo cha Afya Mjimwema kilianzishwa Aprili 8,2002,Kituo hicho kina majengo nane yakiwemo Jengo la wagonjwa wa nje,Wodi ya Watoto na Wanawake,Wodi ya Wazazi na huduma za kujifungua, jengo la kutolea huduma za afya ya uzazi na mtoto na wodi ya Wanaume, jengo la Utawala, jengo la kuhifadhia maiti, nyumba mbili za watumishi na jengo la upasuaji.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa