WAJASIRIMALI wadogo wapatao 380 kutoka vikundi 67 katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wamepata mafunzo ya mbinu za uwekezaji katika viwanda vidogo.
Mafunzo hayo ambayo yamefanyika kwenye ukumbi wa Songea Klabu mjini Songea, yameratibiwa na Idara ya Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Songea,na kufundishwa na watalaam mbalimbali wa Taasisi na asasi za kifedha za serikali.
Akisoma taarifa ya vikundi hivyo,Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii katika Manispaa hiyo,Naftari Saioloyi amesema Manispaa ya Songea imekuwa na utaratibu wa kukopesha vikundi vya wanawake na vijana kutoka katika mapato yake ya ndani.
Amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2017/2018,jumla ya vikundi 102 vilikopeshwa shilingi milioni 116 kati ya hizo vikundi 87 vya wanawake vilikopeshwa Zaidi ya milioni 101 na vikundi vya vijana 15 vilikopeshwa shilingi milioni 14.9.
“Mikopo hii ililenga katika kila kikundi kuendeleza miradi ambayo ilianzishwa.Leo hii Manispaa ya Songea imeona ni vyema viongozi wa wanavikundi kukutana na wataalam toka Taasisi za serikali za SIDO,VETA na wataalam wa Benki ili wapate mafunzo na kuweza kupanua wigo wao wa uwekezaji’’anasisitiza Saioloyi.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yataviwezesha vikundi kutafakari kulingana na maeneo wanayotoka,rasimali walizonazo na upatikanaji wa soko kwa mazao watakayozalisha.
Akizungumza kabla ya kufungua mafunzo hayo,mgeni rasmi Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Mgema amesisitiza kuwa mafunzo hayo ni muhimu hasa katika kutekeleza kauli mbiu ya serikali inayolenga Tanzania ya viwanda na kwa kila mkoa kuwa na viwanda 100.
Amesema kuwa wajasirimali wadogo watakapofanikisha kwenye uwekezaji hata kama ni wa kiwanda kidogo sana,watakuwa kwenye malengo ya Taifa ya viwanda.
“Hakuna aliyezaliwa akaanza kutembea,bali huanzia kutambaa,kusimama halafu kutembea,kiwanda kidogo kinaanza na mtaji mdogo,anzeni sasa na mtayaona mabadiliko’’, anasisitiza Mgema.
Mafunzo ya mbinu za uwekezaji katika viwanda mdogo yametolewa na Taasisi za serikali nchini ambazo ni SIDO,VETA,TCCIA na Benki za NMB,CRDB na POSTA.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Aprili 20,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa